VIGOGO WANNE IMTU KORTINI SAKATA LA MABAKI YA MIILI

Vigogo wanne wa Chuo Kikuu cha Kimataifa Cha Tiba na Teknolojia (IMTU),  wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, wakikabiliwa na mashitaka ya kutupa mifuko 83 yenye miili ya binadamu  kinyume cha sheria.
Washitakiwa hao ambao ni wataalamu na walimu wa IMTU ni Venlat Subbaiah (57), Appm Shankar (64), Prabhakar Rao (69) na Dinnesh Kumar (27).
Walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mawili na Wakili wa Serikali, Magoma Mtani  mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kwey Rusema.
Ilidaiwa kuwa Julai 20 mwaka huu, katika eneo la Mpiga Majohe washitakiwa wakiwa wataalamu na walimu wa IMTU, walishindwa kufukia miili ya binadamu ambayo ni  mifuko 83 kinyume na sheria, miili hiyo ilitumiwa na wanafunzi kwa ajili ya kufanya mafunzo ya vitendo.
Katika mashitaka mengine, vigogo hao wanadaiwa tarehe hiyo hiyo, walishindwa kupeleka hati kwa Ofisa Mchunguzi wa Vifo, kuonesha kuwa wamefukia miili mingapi ya binadamu  na sehemu gani.
Washitakiwa hao walikana mashitaka, ambapo Hakimu Rusema alisema ili washitakiwa wawe nje kwa dhamana, wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili  Watanzania wanaotambulika na Serikali.
Hata hivyo, wakati mchakato wa dhamana unaendelea, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Salum Mohamed aliwasilisha hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwafutia mashitaka washitakiwa hao.
Wakili Mohamed alidai DPP hana nia ya kuwashitaki vigogo hao kwa sasa. Pia,   alidai mashitaka hayo yameletwa mahakamani hapo kimakosa.
Kutokana na hati hiyo ya DPP, Rusema alikubali kuondoa mashitaka hayo na washitakiwa wakaachiwa. Hata hivyo, Jeshi la Polisi liliwachukua tena washitakiwa hao na kuondoka nao.
Nje ya Mahakama, Wakili wa washitakiwa hao, Gaudiosus Ishengoma alisema kitendo hicho cha kuwaachia na kuwakamata tena, kinaashiria kwamba wanataka kuwashitaki wateja wake kwa makosa, ambayo hayana dhamana.

No comments: