UJENZI MUHAS KUONGEZA UDAHILI WA WANAFUNZI

Kukamilika kwa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) na ujenzi wa hospitali ya kisasa katika Kijiji cha Mloganzila, kunatarajiwa kuongeza mara tano ya udahili wa sasa wa  wanafunzi.
Akizungumza jana, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Ephata Kaaya alisema kwa sasa chuo kinadahili wanafunzi 3,000. Ujenzi ukikamilika, kitadahili wanafunzi 15,000 watakaosoma taaluma mbalimbali za afya.
Alisema kukamilika kwa ujenzi huo pia kutatoa fursa kwa wanafunzi kupata sehemu za kusomea kwa ufanisi kama vile ya maabara za kisasa, madarasa, na sehemu za ufanyaji mazoezi.
Hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete aliweka jiwe la msingi kuashiria kuanza ujenzi wa hospitali ya kisasa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili.
Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sylvia Temu alisema ndani ya miaka mitano serikali imewekeza katika elimu ya juu kwa kuboresha miundombinu ya vyuo vya umma.
Temu alitolea mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo wameweza kujenga maabara za sayansi, kuboresha miundombinu katika Kitivo cha Uhandisi na kujenga majengo mapya.
“Ukiangalia vyuo vya umma vilikuwa katika hali mbaya lakini sasa miundombinu yake imeboreshwa na hata Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kilizidiwa na ndio maana serikali inajenga chuo kikubwa,” alisema.

No comments: