TAASISI YA KUFUNDISHA HISABATI YAJA, MKATABA KUSAINIWA AGOSTI 4

Serikali inatarajia kusaini makubaliano ya awali (MOU) na  Taasisi ya Masuala ya Sayansi ya Hesabu Afrika (AIMS), yatakayoiwezesha taasisi hiyo kuanzisha kampasi yake hapa nchini itakayofundisha na kuendeleza masomo ya  Hisabati na Sayansi. 
Katika taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sylivia Temu, mkataba huo utasainiwa rasmi Agosti 4, mwaka huu.
Alisema kampasi hiyo itakuwa ya tano kuanzishwa na taasisi hiyo katika mataifa mbalimbali na itasaidia  kuandaa  wataalamu  wa  kuendeleza masomo  ya Hisabati na Sayansi nchini kwa njia tofauti, ikiwa  ni pamoja  na ufundishaji wa masomo hayo kwenye  ngazi  mbalimbali za elimu. 
“Kuanzishwa  kwa kampasi  hiyo  ni jitihada za  Rais Jakaya  Kikwete, aliyekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa AIMS, Profesa  Nell Turok, ambaye pia ni Mkurugenzi  Mtendaji  wa  Taasisi ya  Perimetr  Institute  for  Theoretical  Physics, ambayo  ina uhusiano na AIMS,” alisema Profesa Temu.
Alisema Profesa Turok ni mzaliwa wa Afrika Kusini na ni mtoto wa Ben Turok, mpigania uhuru wa nchi hiyo ambaye ni mbunge na aliwahi kuishi Tanzania wakati wa utoto wake.
Kwa mujibu wa Profesa Temu, taasisi hiyo inayotoa shahada za utafiti kwa ngazi  mbalimbali, inalenga  kutoa wanafunzi  wenye uwezo  wa  kufanya  utafiti  wenye ubora  wa kiwango  cha juu  katika  masuala ya  sayansi.
Alibainisha kuwa AIMS imejikita  kutoa  mafunzo  katika ngazi ya Uzamili  kwenye sayansi  za Hisabati na hadi mwaka  2013, taasisi hiyo ilishaanzisha vituo  vinne Afrika  katika nchi za  Afrika Kusini, Ghana, Cameroon na Senegal.
“Serikali kwa kutambua umuhimu wa masomo ya Sayansi na mwitikio chanya uliopo sasa kwa wanafunzi kusoma masomo hayo, imeendelea kuimarisha miundombinu ya shule kwa kutoa fedha za ujenzi, ukamilishaji na ukarabati wa majengo ili wanafunzi wengi zaidi wasome masomo hayo,” alisema.
Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wataalamu katika fani za sayansi, kwa kujiwekea mkakati wa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi aliyefaulu masomo ya Sayansi, anapangiwa taasisi ya masomo ya Sayansi.

No comments: