SUMATRA YABARIKI UKATISHAJI TIKETI KWENYE MITANDAO

Mamlaka ya Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) imesema haina pingamizi kwa kampuni zinazotoa huduma ya usafiri wa mabasi kwenda mikoani kutumia mfumo wa kuuza tiketi kwa njia ya mtandao.
Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Sumatra, David Mziray  alisema hayo akijibu hoja iliyotolewa na Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua) kuwa mamlaka hiyo imekuwa kikwazo cha kutumia mfumo wa kukata tiketi kwa njia ya mtandao.
Mziray alisema  kampuni ambayo iko tayari kutumia mfumo huo inaruhusiwa ili mradi itoe tiketi halali na kwa bei halali.
“ Sisi hatuna tatizo, mmiliki anayetaka kutumia afanye hivyo. Sheria haitulazimishi kusimamia mfumo upi utumike kukata tiketi ila tunachotakiwa ni kuhakikisha tiketi inayotolewa ni halali kwa bei halali,” alisema.
Awali, Mwenyekiti wa Chakua, Hassan Mchanjama alisema: “Tumefuatilia utekelezaji wa ukataji wa tiketi za mabasi ya kwenda mikoani kwa njia ya ya mtandao ikiwamo simu na mkononi kwa muda mrefu bila mafanikio,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) Enea Mrutu alisema pamoja na wanachama wao kuruhusiwa kutumia mfumo, utekelezaji wake ni mgumu.
“Lakini utekelezaji wake umekuwa ni mgumu kutokana na baadhi ya watoa huduma, kutokuwa wanachama wetu na pia wengine wanaogopa uharamia,” alisema.

No comments: