RAIS SHEIN KUHUTUBIA BARAZA LA EID

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein atalihutubia Taifa katika Baraza la Eid katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana, sala ya Idd kitaifa itafanyika katika Msikiti Mkuu wa Mwembe Shauri.
Taarifa hiyo ilisema Baraza la Idd , litahudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi na litafanyika katika Hoteli ya Bwawani.
Ofisa wa Wakfu na Mali ya Amana, aliyejitambulisha kwa jina moja la Haji alisema maandalizi ya Baraza la Idd yamekamilika, ambapo Waislamu mbalimbali kutoka mikoa mitano ya Unguja wamealikwa.
Kwa kawaida hotuba ya Baraza la Idd, hutumiwa na viongozi wakuu kuelezea masuala mbalimbali, ikiwemo hali ya nchi na ustawi wa jamii.
Kwa wiki moja sasa, baadhi ya wananchi  walikuwa katika maandalizi ya Sikukuu ya Idd huku wazazi wakitafuta bidhaa mbali mbali ikiwemo chakula na nguo kwa ajili ya watoto.
Mwandishi aligundua kwamba bidhaa za nguo, zimepanda maradufu mwaka huu, kiasi baadhi ya wananchi kulazimika kufunga safari kwenda Tanzania Bara kununua bidhaa hizo.
“Bidhaa za nguo za watoto zimepanda bei zaidi mwaka huu na wazazi wengi wameenda Dar es Salaam kwa ajili ya kununua nguo ambazo zinapatikana kwa bei nafuu,” alisema Fatuma Haji, mkazi wa Zanzibar.
Bei ya nguo za watoto zimepanda na kufikia Sh 40,000 kwa kuanzia, hadi Sh 100,000. Hata hivyo bidhaa za nguo za mitumba zimekuwa zikipatikana kwa wingi na kwa bei nafuu.

No comments: