POLISI KUTUMIA MAGARI YA WASHAWASHA KUDHIBITI VURUGU IDD EL FITRI

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya Ulinzi na Usalama imeimarisha ulinzi ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea Sikukuu ya Idd el Fitr kwa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema zitafanyika doria za miguu, pikipiki na magari ya washawasha, askari wa mbwa na farasi ili kuhakikisha usalama.
“Tutashirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, kampuni binafsi za ulinzi, vikosi vya uokoaji wakati wa majanga na vikundi vya ulinzi shirikishi kuhakikisha kuna udhibiti wa matukio ya uhalifu au fujo zinazoweza kujitokeza,” alisema.
Aidha, alisema kuwa kutokana na sababu za kiusalama na matishio mbalimbali katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki, jeshi hilo limepiga marufuku disko toto katika kumbi mbalimbali kutokana na sifa za kumbi hizo kutokidhi viwango vya kiusalama.
“Wananchi wanapoona dalili zozote au maandalizi ya uvunjifu wa amani watoe taarifa mapema iwezekanavyo katika vituo vya Polisi vya karibu ili hatua zichukuliwe haraka,” alisema Kova.
Alisema madereva wote wanatakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kutoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi na kutokutumia kilevi.
Pia alisema Kikosi cha Polisi Wanamaji kitafanya doria kwenye fukwe za bahari na maeneo yote ya bahari jijini humo ambapo pia helikopta ya Jeshi la Polisi itafanya doria kuzunguka jiji hilo.
“Polisi watatoa ulinzi maalumu katika fukwe za bahari kwa kuweka vituo vya Polisi vya muda vinavyohamishika ili kutoa msaada wa haraka pindi unapohitajika. Pia askari wa kutosha watakuwepo kuhakikisha wananchi wanasherehekea kwa amani,” alisema Kamanda Kova.

No comments: