MFUKO WA RAIS WAELEZA SABABU ZA MIKOPO KUTOTOLEWA

Mfuko wa Rais (PTF) Kanda ya Morogoro umeshindwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali pamoja na Vyama vya Kuweka na Kukopa  (Saccos) kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na baadhi  kushindwa kurejesha mikopo.
Mikopo hiyo iliyotolewa mwaka  2009/2010 hali iliyosababisha kuwanyima fursa wajasiriamali pamoja na Saccos zilizorejesha kushindwa kupata fedha hizo.
Meneja wa PTF Kanda ya Morogoro, Christopher Peter alisema hata hivyo juhudi zimefanyika kuhakikisha madeni yanalipwa.
Kutokana na juhudi hizo,  hivi sasa Saccos moja pekee ndiyo inadaiwa kutokana na kushindwa kurudisha hata nusu ya deni.
Meneja huyo alitaja Saccos hiyo kuwa ni Ushirikiano inayodaiwa Sh milioni  22.1 walizozichukua katika kipindi cha mwaka 2009/2010.
Peter alisema  fedha hizo ni za wananchi na anashangaa kuona taasisi husika zikishindwa kurejesha fedha hizo ambazo kila mwananchi mwenye uhitaji aliyeidhinishwa na Mfuko anapaswa kukopa na kurejesha kwa wakati.
Hata hivyo alisema mpango wa kuendelea kutoa mikopo kwa Saccos uko palepale. Alisisitiza kabla ya kutoa mikopo hiyo, watazichambua na kuzifanyia usaili.
Kwa mujibu wa Peter, Sh milioni 424.9 zilikopeshwa kwa Saccos katika kipindi hicho cha mwaka 2009/2010.

No comments: