MBOWE, SLAA KUTETEA NAFASI ZAO UCHAGUZI WA CHADEMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa rasmi ratiba yake ya uchaguzi wa ndani, ambapo viongozi wa taifa wa chama hicho, akiwemo mwenyekiti na katibu mkuu wapya wanatarajiwa kutangazwa Septemba 11, mwaka huu.
Pia chama hicho kimesema Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe na Katibu wake Mkuu, Dk Wilbroad Slaa, wanayo haki ya kuendelea kutetea nafasi zao hizo kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Kampeni za Uchaguzi wa chama hicho, Singo Kigaila, alisema ratiba hiyo, ilitolewa na kuthibitishwa na Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi Julai 18 hadi 20, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
 “Tunafahamu kuwa Dk Slaa alishatangaza ratiba nyingine ya uchaguzi wa ndani na kubainisha kuwa uchaguzi wa ngazi ya taifa utafanyika Agosti 30, mwaka huu, lakini kutokana na wageni wetu tuliowaalika na mipango kuingiliana tumeahirisha uchaguzi huo, hadi Septemba 14,” alisema Kigaila.
Alisema kwa mujibu wa kamati hiyo, pia iliidhinisha ratiba ya chaguzi zingine za ndani za chama hicho, ambapo iliazimia kuwa uchaguzi wa Baraza la Wazee Taifa utafanyika mapema zaidi  kuwezesha kusimamia uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya taifa kama Katiba ya chama hicho inavyotaka.
“Kamati pia imeazimia uchaguzi ngazi ya Kanda utafanyika baada ya uchaguzi wa ngazi ya taifa, ili kuwezesha mkutano mkuu kufanya maboresho ya Katiba ya chama hicho, kwa ajili ya kuwezesha ngazi hiyo kufanya uchaguzi kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Alisema ratiba hiyo mpya inaonesha kuwa uchaguzi wa kata wa chama hicho utakamilika keshokutwa, uchaguzi wa majimbo na wilaya utakamilika Agosti 15, mwaka huu na uchaguzi wa Baraza la Wazee wa chama hicho utakamilika Septemba 6, mwaka huu.
Aidha alisema Ratiba hiyo pia inaonesha kuwa uchaguzi wa Baraza la Vijana wa Chadema utakamilika Septemba 10 na kufuatiwa na uchaguzi wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), Septemba 11, mwaka huu.
Uchaguzi wa Kamati Kuu ya chama hicho utakamilika Septemba 12 na kufuatiwa na uchaguzi wa Baraza Kuu Septemba 13 huku uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa chama hicho ukifuatia Septemba 14, mwaka huu na uchaguzi wa Baraza Kuu utakamilika Septemba 15 na kumalizia na uchaguzi wa Kamati Kuu mpya Septemba 16, mwaka huu.
Kigaila alisema  Kamati Kuu ya chama hicho, imeagiza kuundwa kwa kamati ya kusimamia uchaguzi wa ndani wa chama hicho ngazi ya mikoa, wilaya na majimbo kwa mujibu wa Katiba ya Chadema.
Alisema tayari fomu za kuwania nafasi hizo zimeanza kusambazwa kwenye ngazi husika ambapo fomu za kuwania nafasi za ngazi ya taifa zitatolewa kwa Sh 50,000, ngazi ya mikoa Sh 20,000 na ngazi ya jimbo na ngazi nyingine za chini Sh 10,000.
Kaimu Mwenyekiti wa Bawacha,  Susan Lyimo, alitaka wanawake wanachama wa chama hicho, kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo ya uchaguzi wa ndani wa Chadema kuwania nafasi mbalimbali na kuachana na tabia ya kuwa wasindikizaji.

No comments: