MANISPAA YA KINONDONI YATIMUA KAZI WATUMISHI WAKE

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imewafukuza kazi watumishi tisa wa idara mbalimbali kutokana na makosa ya utoro kazini pamoja na matumizi mabaya ya madaraka ya ofisi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Uhusiano wa Manispaa hiyo, Sebastian Mhowera mbali na hatua hiyo pia imewapa karipio watumishi wengine wawili kutokana na makosa hayo.
Alisema hatua hiyo ilifikiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo kilichokaa Julai 22 mwaka huu chini ya Mstahiki Meya Yusuph Mwenda ambacho mbali na mambo mengine kilijadili na kutoa maamuzi ya mashitaka ya nidhamu yaliyofunguliwa kwa watumishi 11.
“Baraza limefikia uamuzi wa kuwafukuza kazi watumishi 9 na kuwapa karipio watumishi wawili, kati ya watumishi waliofukuzwa kazi wanatoka idara za afya, utawala na utumishi, wamo maofisa watendaji wa mitaa, walimu kutoka idara ya elimu ya sekondari na polisi msaidizi mmoja,” alisema Mhowera.
Aidha alisema watumishi wawili waliopewa karipio kutoka Idara ya afya wametakiwa kujirekebisha na watakuwa katika uangalizi kwa muda kuona kama watajirekebisha mienendo yao.

No comments: