MAKANISA YANAYOENDEKEZA VURUGU KUFUTILIWA MBALI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amesema yeye mwenyewe atayafuta makanisa yote yanayoleta vurugu na uvunjifu wa amani kwa kuwa hayatoi taswira ya kile wanachopaswa kufanya na ni aibu kwa Mungu  wanayemtumikia.
Amesema ni aibu kwa viongozi wa makanisa kupigana hadharani wakati wa Ibada na kupishana katika vituo vya Polisi wakishtakiana jambo alilosema linachochea shari na kuharibu nchi.
Amelitaja kanisa mojawapo ambalo lina vurugu kuwa ni Kanisa la Moravian, Jimbo la Misheni Mashariki ambalo kwa zaidi ya miaka miwili sasa sharika zake zimekuwa na vurugu inayohusisha uongozi na ubadhirifu wa mali.
"Serikali haitavumilia vitendo vya vurugu katika makanisa na ikibidi mimi mwenyewe nitayafuta usajili wa hayo makanisa yenye migogoro kuepusha shari," alisema Chikawe jana katika ibada maalumu ya kuombea Taifa amani, utulivu na uzalendo wa kweli.
Hivi karibuni kanisa hilo wilayani Kinondoni, waumini walipigana na sasa kuna kesi kuhusu ugomvi huo katika vyombo vya Sheria.
Maombi hayo yaliandaliwa na Chama cha Kitume cha Karismatiki Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kufanyika katika viwanja vya Kituo cha Maombi na Maombezi cha Emaus, kilichopo Ubungo, jijini humo.
Chikawe aliyekuwa mgeni rasmi akiwakilisha viongozi wa Serikali na kisiasa katika maombi hayo yaliohusisha pia kuombea mchakato wa Katiba, vita dhidi ya rushwa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani, alisema viongozi wa dini wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kuchochea amani ya Taifa, lakini inashangaza baadhi yao wanaongoza kwa kuleta vurugu.
"Kwa bahati mbaya migogoro katika makanisa na madhehebu mbalimbali imekuwa mingi wakati huu na sababu za migogoro hiyo ni pamoja na ubinafsi wa viongozi, kutofuata Katiba na ubadhirifu wa mali za kanisa, mathalani Kanisa la Moravian Tanzania, lipo katika mgogoro mkubwa hivi sasa kiasi cha watu kupigana hadharani.
"Wanapigana wakati wa ibada, tujiulize ni mfano gani tunawaonesha Watanzania wasio na dini, kwa utaratibu huo nani atatamani kuwa Mkristo, natumia fursa hii kuwakumbusha viongozi kuwa mfano wa kuigwa, viongozi ni  lazima  tuwe na hofu ya Mungu na tutumie nafasi zetu kujenga umoja, amani na mshikamano," alisema Chikawe.

No comments: