KESI YA ARV'S FEKI YAPIGWA KALENDA HADI SEPTEMBA 3

Kesi ya kusambaza dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs) inayomkabili Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha Tanzania Pharmacentical Ltd ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, inatarajiwa kuendelea kusikilizwa Septemba 3 mwaka huu.
Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka ambaye aliahirisha hadi Septemba 3 kwa ajili ya kusikiliza mashahidi wa upande wa mashitaka, kwa kuwa Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba  anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo mahakamani.
Mbali na kushitakiwa kwa kusambaza dawa hizo, Madabida na wenzake wanadaiwa kusababisha hasara ya Sh milioni 148 baada ya kusambaza dawa hizo kupitia kiwanda chake cha TPL kwa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD).
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni wafanyakazi wa kiwanda hicho Mkurugenzi Uendeshaji, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msoffe na Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango, pamoja na wafanyakazi wa MSD, Meneja Udhibiti Ubora, Sadick Materu na Ofisa Udhibiti Ubora, Evans Mwemezi.
Inadaiwa Aprili 5 mwaka 2011, Madabida, Shamte, Msoffe na Fatma walisambazia MSD makopo 12,252 ya dawa bandia za Antiretroviral, ikionesha zimetengenezwa Machi 2011 na mwisho wa matumizi Februari mwaka jana pia walijipatia Sh milioni 148.35 kwa madai ni malipo halali ya dawa hizo.
Materu na Mwemezi wanadaiwa, kati ya Aprili 5 na 13, 2011, Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa MSD, kwa nia ya kutenda kosa la kusambaza dawa hizo, walishindwa kutumia uwezo wao wote kuzuia kutendeka kwa kosa hilo.
Katika mashitaka mengine, washitakiwa wote wanadaiwa kati ya Aprili 5 na 30, mwaka 2011, kwa nia ovu au sababu za kutotekeleza majukumu yao vizuri, waliisababishia MSD hasara ya kiasi hicho cha fedha, kutokana na kuwasambazia dawa bandia.

No comments: