KAMPUNI ZATAMANI KUINGIA UBIA NA ATCL

Kampuni kubwa za ndege zimeonesha nia ya kuja nchini kuingia ubia na Kampuni ya Ndege nchini (ATCL) kuongeza ufanisi na ushindani wa biashara katika usafirishaji wa anga.
Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe amewahakikishia wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kuwa ndani ya miezi mitatu ijayo kuanzia sasa, ATCL itakuwa imebadilishwa katika uendeshaji wake.
Alisema hivi karibuni anatarajia kwenda nchini Marekani ambako pamoja na mambo mengine, atapata fursa ya kufanya mazungumzo na mwekezaji wa nchini humo ambaye ameonesha nia ya kufahamu kuwekeza katika usafiri wa anga.
“Katika kipindi kirefu ATCL, imepitia katika misukosuko mingi ikiwemo wizi, ubabaishaji, rushwa lakini baada ya kurekebisha hesabu ya mizania mashirika mengi ya kimataifa yanataka kuwekeza katika ATCL ili kuleta ushindani katika usafiri wa anga,” alisema Dk Mwakyembe.
Alikuwa akizungumza na wafanyakazi wa TCAA mwishoni mwa wiki ambapo pia alizindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo itakayofanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu kwa mujibu wa sheria.
Akijibu swali la mmoja wa wafanyakazi, Mtesigwa Maugo aliyetaka kufahamu kuhusu uboreshaji na usimamizi wa usafiri wa anga, Dk Mwakyembe alisema wawekezaji kutoka Marekani na Oman wameonesha dhamira ya kuja nchini kuingia ubia na ATCL.
Waziri Mwakyembe aliahidi kutatua kero  ya muda mrefu ya wafanyakazi wa TCAA  na wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)  kutakiwa kulipa Sh  50, 000 kwa mwaka kama tozo ya magari yao yanapoingia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nyerere (JNIA).
Dk Mwakyembe alimwelekeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, kumpelekea kwa maandishi malalamiko yote ya wafanyakazi ayatafutie ufumbuzi na kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi mkubwa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Charles Chacha alisema Sekta ya Usafiri wa Anga nchini haijakua. Alitoa mfano wa mashirika ya ndege nchini kuwa hayajaweza kushindana na mashirika mengine ya kimataifa.
Alitaja changamoto inayoikabili  mamlaka kwa sasa kuwa ni ya usimamizi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa wanataaluma hasa wakaguzi.
Hata hivyo alisema juhudi zinachukuliwa  kurekebisha kasoro zilizojitokeza; ikiwa ni pamoja na kuajiri kwa mikataba ya muda mfupi wakaguzi waliostaafu na wengine kutoka katika sekta hiyo.

No comments: