KAMPUNI YA NAKUMATT KUNUFAISHA WAFANYABIASHARA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nakumatt Holdings Limited, Atul Shah amewahakikishia Watanzania kunufaika na duka jipya la vyakula na vifaa kwa kupata fursa mbalimbali ikiwamo kununua bidhaa za wafanyabiashara wa hapa nchini.
Shah aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa duka hilo lililopo Mlimani City, ambapo alihakikisha kuwa duka hilo halijaja kuwa maadui wa Watanzania kwa kuwanyang'anya fursa zao ikiwemo ajira.
Alisema duka hilo litahakikisha linanunua bidhaa zake kwa wafanyabiashara wa hapa nchini kusaidia kuleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa bidhaa zitakazokuwa na viwango vya kimataifa zitapata fursa za kuuzwa katika maduka yao mengine yaliyopo nchi za Afrika Mashariki.
Alisema walikuwa na ndoto za muda mrefu za kufungua duka hilo jijini hapa na kwa sasa imekamilika, ambapo alisema kuwa mikakati waliyojiwekea ni kuwa na matawi 50 Afrika Mashariki kufikia mwaka 2015.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene ametaka wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nchini kuhakikisha wanatumia vizuri fursa zilizopo ili kurasimisha biashara zao na kuongeza kipato.
Mbene alisema, wajasiriamali wadogo wana uwezo mkubwa wa kutengeneza bidhaa bora lakini wamekuwa wakiangushwa na utafutaji wa masoko.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa duka la vyakula na vifaa la Nakumatt,  Mbene alipongeza uamuzi wa duka hilo wa kuhakikisha linanunua bidhaa zake hapa nchini kwa lengo la kuongeza maendeleo.
Alisema tofauti na maduka mengine ambayo asilimia kubwa ni ya nchi za mbali, duka hilo ni kutoka ndani ya Afrika Mashariki hivyo ujio wa duka hilo ni fursa nzuri kwa Watanzania.
Alitaka wajasiriamali kuhakikisha wanatengeneza bidhaa zenye viwango vya kimataifa kama walivyofanya katika Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba' waweze kupata soko kubwa na kufanya kutoka katika sekta isiyo rasmi kwenda katika sekta rasmi.

No comments: