CHUO KINGINE CHA TIBA MATATANI, CHAPIGWA MARUFUKU

Siku moja baada ya Serikali kuifungia kwa muda usiojulikana Hospitali ya Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU), kinachohusishwa na utupaji wa viungo vya binadamu mithili ya takataka, Serikali mkoani Rukwa nayo imekifungia chuo kingine cha  Rukwa College of Health and Allied Sciences.
Moja ya sababu ya kukifungia chuo hicho ni kutokuwa na kibali cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii huku mitaala ya kozi zake ikiwa haipo, kwa maana ya kupitwa na wakati.
Kutokana na kasoro hizo, Serikali ya mkoa kupitia Idara yake ya Afya imezuia wanafunzi wa chuo hicho kufanya mazoezi ya vitendo katika Hospitali ya Mkoa na nyingine mkoani hapa.
Chuo  hicho kinachomilikiwa  na Umoja wa Kuendeleza Wanawake Mkoani Rukwa (RWAA)  ambacho kipo  Kanondo, nje kidogo  ya Mji wa Sumbawanga, kwa sasa wanafunzi  wake wa mwaka  wa mwisho wako katika maandalizi ya mitihani yao  ya  kuhitimu  masomo. Mitihani hiyo inatarajia kuanzia Agosti 25, mwaka  huu.
Mganga Mkuu  wa Mkoa wa Rukwa, Dk John Gurisha  amelithibitishia gazeti hili juu ya uamuzi huo wa serikali ya mkoa kwa kile alichosema chuo hicho kinaendeshwa  kinyemela,  ikiwa ni  kinyume cha utaratibu  kwani hata  mitaala ya kozi  zinazofundishwa haipo katika mfumo wa masomo Tanzania,  hivyo si  rahisi kupata  viwango  vya ubora  wa  wanafunzi.
Akifafanua,  Dk Gurisha  alisema  usajili  wa muda   uliotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NACTE) haukipi chuo hicho  uhalali  wa kutoa  mafunzo ya tiba,  bali  kinatoa  ruhusa ya kufungua  chuo ili kiweze kutoa  kozi  za  tiba.
Alisema baada ya kupata usajili huo, chuo kilitakiwa kupata kibali kutoka kwa Katibu Mkuu  Wizara ya Afya  na Ustawi  wa Jamii  na si vinginevyo.
 Aliongeza kuwa   chuo hicho hakifuati  mitaala  ya Wizara ya Afya kwa kuwa  kozi ya  wahudumu wa afya   inayotolewa  chuoni  hapo ilishasitishwa na wizara husika.
“Awali  kabla Wizara  ya Afya na Ustawi  wa Jamii  kusitisha  kozi  ya  wahudumu wa  afya  ilikuwa ikitolewa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa pekee  kwa mantiki hii  kozi  zinazofundishwa  chuoni  hapo ni batili,  pia hakina  baraka za Katibu Mkuu  wa Wizara ya Afya  ambaye  ndiye  pekee  mwenye mamlaka  ya kutoa  vibali vinavyowezesha vyuo  vya afya  kufundisha  kozi mbalimbali.
“Hivyo chuo  hiki  akitambuliwi,  nimezuia pia  wanafunzi  wa chuo hicho kufanya  mazoezi ya vitendo  katika hospitali  hii ya mkoa na zinginezo  zilizopo  mkoani hapa;  sasa  kutokana  na hili  chuo hicho kinawapeleka wanafunzi wake Mpanda  mkoani Katavi  kwa  mafunzo  ya  mazoezi kwa  vitendo …. Niwe wazi wanaosoma katika chuo hicho wanajipotezea muda wao,“ alisema.
Aliongeza kuwa  atahakikisha  chuo  hicho  kinafuata utaratibu   ili kiweze kutambuliwa na kwamba haogopi  licha  ya kauli kali  zinazomshutumu  kuwa  yeye (Dk Gurisha)  anakipiga vita kwa kuwa  si mzawa  wa  mkoa huo.
“Huwezi  kuchezea  maisha na afya za watu kwa  sura ya uzawa …kwanza kama  kweli  kingekuwa  ni halali  ilikuwa ni jambo jema  kwetu kwa kuwa  baadhi ya wahitimu  wake  wangeweza kuajiriwa hospitalini hapa na kwingineko   ili kupunguza  upungufu wa wahudumu  wa afya wenye ujuzi,“ anaeleza.
Naye Katibu  wa Hospitali  ya Mkoa wa Rukwa, Dorice Nzingilwa  anasema  wanafunzi wa chuo hicho  wanasoma  kwa  miezi  mitatu kisha wanapelekwa  kufanya  mazoezi  ya vitendo  na kuanza  kuwatibu wagonjwa,  jambo  ambalo linahatarisha  maisha ya wagonjwa.
Aidha alisema hata walimu wanaofundisha  katika  chuo hicho hawana  sifa  kwa kuwa baadhi yao  ni  matabibu wasaidizi.
Kwa mujibu  wa  barua  ya Agosti 20, 2013  iliyosainiwa na Dk Gurisha kwenda  kwa Katibu Mkuu  Wizara ya Afya  na Ustawi wa Jamii yenye kumbukumbu namba GHS /T 40/15/4,  licha ya kuainisha mapungufu lukuki yanachokikabili  chuo  hicho  pia  kimebainisha kuwa  kinaendeshwa kinyume cha utaratibu  kwa vile hata mitaala  ya kozi  zinazofundishwa  haipo .
“Hivyo  si rahisi kupata  viwango  na ubora wa wanafunzi,“ inaeleza sehemu ya  barua  hiyo.
Pia imebainisha kuwa Kaimu Mkuu  wa Chuo  hicho ni Ofisa  Tabibu mstaafu  na wengine watatu ambao  ni walimu wa kudumu  ni  wauguzi wastaafu  huku mwingine  cheo chake pia makazi  yake halali hayafahamiki. 
Pia kwa mujibu wa barua  hiyo  walimu  wa muda ambao ni watano hawafai kufundisha kwani mmoja wao ni muuguzi mstaafu, wengine tabibu wasaidizi  watatu na daktari mmoja kutoka Hospitali ya Rufaa  ya Mkoa  wa Rukwa.
“Timu ya usimamizi wa huduma  za afya  Mkoa RHMT na ile ya wilaya CHMT  tunapendekeza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii  iwe inafanya ukaguzi wa vyuo  vinavyotaka kuanzishwa  kabla ya Nacte ili wajiridhishe;  na wakati wa  kufanya  ukaguzi  washirikishe timu ya mkoa  na wilaya ili  kuondoa  au kuepuka  migongano isiyo ya lazima  kati ya Wizara  ya Afya na Nacte  wataarifiwe  kwa ajili ya kukamilisha  usajili. Aidha Nacte  wafahamishwe  kwamba  wanapotoa usajili  msimamizi mkuu  na mtoa mitaala  ni Wizara  husika …
“Na ukaguzi wanaoufanya Nacte  uzingatie  vigezo  vilivyopo  kwani hatutegemei  kama Rukwa College  of Health Sciences  wangepewa  namba ya usajili  kwa hali  tuliyoikuta  wakati wa  ziara yetu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Akizungumzia hayo, Mwenyekiti  wa Asasi  hiyo ya RWAA  inayomikili chuo hicho, Annastela Malaji  anasititiza kuwa  chuo  hicho  ni halali kwa kuwa  kimepata usajili  wa muda  kutoka Nacte uliotolewa Januari 31,2014  na kitakoma Januari 30,2015 ambapo  kilishaanza kuchukua wanafunzi tangu mwaka  jana.
“Tuko kihalali  isitoshe tuna usajili wa Nacte  kama kweli  tungekuwa hatuna uhalali  mbona Agosti 25 mwaka  huu  wanafunzi  watafanya mitihani yao  ya kuhitimu  tena wataifanyi katika hospitali  ya mkoa kwa  maelekezo ya Wizara  husika …. Lipo jambo  hapa,“  alisema Malaji.
 Katika hatua nyingine, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimepongeza uamuzi wa Serikali wa kuifungia Hospitali ya Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU) na kuiomba kufanya ukaguzi kwa hospitali nyingine nchini za serikali na binafsi.
Hayo yamesema na Rais wa MAT, Dk Primus Saidia aliyeongeza kuwa, hatua ya serikali inalinda watu wake na kuhakikisha watoa huduma wanakuwa na sifa stahili, huku wakitoa huduma bora.
Alisema kutokana na taaluma ya afya kuingiliwa na matatizo mbalimbali, ikiwemo kuwepo kwa watoa huduma wasio na sifa huku wengine wakiwa hawana vifa vya kutosha hivyo ukaguzi uendele na hospitali nyingine.
“Tunaipongeza serikali kwa hatua hii ya kumlinda mlaji, lakini tunawasihi isiwe kwa IMTU pekee kwani kuna hospitali za binafsi na za serikali zenye matatizo kama ya IMTU na zinatakiwa kuchukuliwa hatua,“ alisema Dk Saidia.
Alisisitiza kuwa pia inatakiwa kuzingatia hospitali zote zinakuwa na namna ya kutupa na kuteketeza taka za hospitalini kwa ajili ya kulinda afya za wananchi wake kwani uchafu kama damu au mabomba yaliyotumika yana madhara mbalimbali.
Rais huyo wa MAT, aliwataka wananchi wanaopatiwa huduma zisizoridhisha katika hospitali na vituo mbalimbali vya afya nchini kupeleka malalamiko yao ili hatua ziweze kuchukuliwa, jambo litakalosaidia kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo muhimu.

No comments: