BARABARA 12 ZANZIBAR ZAKARABATIWA

Bodi ya Mfuko wa Barabara Zanzibar umezifanyia ukarabati barabara 12 za mjini na vijijini, kwa lengo la kuimarisha huduma za usafiri kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bodi hiyo, Shomari Omar alisema barabara zilizopo Mji Mkongwe za Mkunazini na Kikwajuni, zimefanyiwa ukarabati kwa kuwekewa kifusi.
Aidha alisema barabara za Mbweni hadi Chukwani na Buyu zimefanyiwa ukarabati na sasa zinapitika kwa urahisi kiasi ya kuimarisha huduma za usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo.
“Bodi ya Mfuko wa Barabara imeweka malengo ya kuzifanyia ukarabati barabara za mjini na vijijini kwa kiwango kikubwa kinachoelekea baadaye kuwekwa lami,” alisema Omar.
Omar alisema malengo ya pili ya bodi hiyo ni kuzifanyia ukarabati barabara za vijijini zaidi katika maeneo ya sekta ya utalii.
Alitaja barabara za vijijini zilizofanyiwa ukarabati kuwa ni Cheju hadi Unguja Ukuu, ambayo hadi kumalizika kwake itasaidia kuimarisha huduma na shughuli za kilimo.
Ofisa wa bodi hiyo, Mohamed Said alisema  Sh bilioni saba zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara hizo.
Said alisema katika awamu ya kwanza, bodi imeweka malengo ya kuzifanyia ukarabati barabara zote za Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwamo ya Mji Mkongwe ambako ni kitovu cha sekta ya utalii.

No comments: