ZAIDI YA NYUMBA 700 BARABARA YA ARUSHA-MOSHI KUBOMOLEWA

Zaidi ya nyumba 700 zilizopo kando ya barabara ya Arusha-Moshi, zitabomolewa  kupisha ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha hadi mpaka wa Holili,  kwa upande wa Tanzania na Taveta hadi Voi nchini Kenya.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa barabara hiyo jana, Meneja wa Wakala wa Barabara(Tanroads) Mkoa wa Arusha, Deusdedit Kakoko, alisema mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB), utaanza kutekelezwa kabla ya Desemba mwaka huu.
Alisema tayari wenye nyumba ambazo zitabomolewa, wameshataarifiwa juu ya suala hilo.
Aliwataka wananchi ambao wameshalipwa fidia zao, kuondoa majengo yao, kabla ya kubomolewa na wakala huo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, aliwataka wananchi wa Arusha kutoa ushirikiano wa kutosha kwenye ujenzi wa barabara hiyo, kutokana na umuhimu wake kiuchumi.
"Mradi huu una umuhimu mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya mkoa wa Arusha, hivyo wananchi wanatakiwa kuunga mkono ili uweze kukamilika kwa wakati,” alisema  Mulongo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale, alisema ujenzi huo unahusisha upanuzi wa barabara ili iwe na njia nne kutoka eneo la Sakina hadi Usa River.
Mfugale alisema mradi huo, utatekelezwa kwa awamu mbili, ikiwemo Sakina-Tengeru (km 14.2) na barabara ya pembeni mwa jiji la Arusha (km 42). Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa kipande cha Tengeru-Usa River (km 8.1) na kisha marekebisho ya barabara hiyo hadi Holili.
Mfugale alisema ujenzi wa barabara hiyo na nyingine ni sehemu ya Mpango wa Uendelezaji wa Mtandao wa barabara za Afrika, ambao nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki(EAC) waliuandaa.
Mhandisi Mwandamizi wa masuala ya Uchukuzi kutoka AfDB, Patrick Musa, alisema barabara ya Arusha-Holili/Taveta-Voi, itakuza biashara mingoni mwa nchi wanachama wa EAC.

No comments: