WAZIRI WA FEDHA KUJIBU HOJA ZA WABUNGE KUHUSU BAJETI LEOLeo Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salumu, anatarajiwa kujibu hoja za wabunge kuhusu makadirio ya bajeti ya Serikali ya Sh trilioni 19.8.
Tofauti na utaratibu wa kawaida wa Waziri kujibu hoja hizo kwa kusaidiana na Naibu mawaziri wake na mawaziri wengine, leo Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge, atatoa taarifa ya mabadiliko ya makadirio ya Bajeti ya Serikali. 
Mabadiliko hayo, yanatarajiwa kupunguza mafungu katika baadhi ya sekta na maeneo, yaliyokuwa yametengewa fedha katika makadirio ya awali ya Bajeti, na kuongezwa katika sekta nyingine.
Mbali na mabadiliko hayo, pia kuna baadhi ya vyanzo vya mapato, vitakuwa vimeongezewa mzigo kutoa zaidi fedha na vingine kupunguziwa mzigo kwa kupunguziwa makato.
 Tayari Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, jana aliwatangazia wabunge wote, wakiwemo waliosafiri wengi wao kwenda Dar es Salaam, kuhudhuria bungeni leo, kwa kuwa wataitwa mmoja mmoja kwa majina yao wakati wa kupitisha bajeti hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mbunge wa Magu, Dk Festus Limbu (CCM), akizungumza na gazeti hili jana, alisema mabadiliko katika mapendekezo ya Bajeti ya Serikali, yanatokana na mazungumzo yaliyofanyika kati ya kamati hiyo, Serikali, wizara mbalimbali na wadau wengine.
Kwa mujibu wa Dk Limbu, awali wizara, idara na taasisi za Serikali, zilipeleka katika Wizara ya Fedha maombi ya Bajeti ya Sh trilioni 29, ambayo Waziri Saada alipoelezea mwelekeo wa Bajeti jijini Dar es Salaam, alikiri maombi hayo yalisababisha utengenezaji wa Bajeti ya Sh trilioni 19.8, kuwa mgumu.
Dk Limbu alisema tangu Serikali isome Bajeti yake bungeni, Kamati ya Bajeti ilianza vikao na wizara, idara na taasisi za Serikali kupata taarifa kwa nini zilipeleka maombi ya Sh trilioni 29, ambazo ni zaidi ya Sh trilioni 10 ya Bajeti iliyotangazwa.
Katika mazungumzo hayo, ambayo Wizara ya Fedha ni sehemu ya majadiliano, Dk Limbu alisema Kamati ya Bajeti, iliamua kufanya mabadiliko katika baadhi ya maeneo, kwa kuyapunguzia fedha zilizokuwa zimepangwa awali.
Aidha, baadhi ya maeneo ambayo yalipangiwa fedha kidogo kwa mujibu wa Dk Limbu, yameongezewa fedha na mabadiliko hayo yatajulikana leo.

Mwandishi alitaka kujua kama baadhi ya vyanzo vya mapato vitakuwa vimeguswa, kwa maana ya kuongezewa mzigo wa kodi au kupunguziwa, ambapo Dk Limbu alisema hata huko katika vyanzo vya mapato, Kamati ya Bajeti imefanya mabadiliko.
Alipoulizwa kama kuna uwezekano wa taarifa ya mabadiliko ya Kamati ya Bajeti, kutofautiana na taarifa ya Waziri wa Fedha, Dk Limbu alisema tofauti zinaweza zisiwepo na zikiwepo ni kidogo, kwa kuwa mabadiliko hayo ni sehemu ya makubaliano kati ya Kamati ya Bajeti na Serikali.
Wakati akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bajeti, mara baada ya Bajeti ya Serikali kuwasilishwa bungeni, miongoni mwa mambo aliyozungumzia Chenge, ilikuwa kodi ya mishahara (Paye).
Chenge alibainisha kuwa Kamati yake, haijaridhishwa na uamuzi wa kupunguza Paye kwa asilimia moja, kutoka asilimia 13 katika mwaka wa fedha unaoisha 2013/2014 hadi asilimia 12 kwa mwaka ujao wa fedha, 2014/2015.
Aliitaka Serikali katika Bajeti  hiyo ya mwaka 2014/2015, ipunguze hadi kufikia tarakimu moja, yaani chini ya asilimia 10, hoja ambayo pia iliungwa mkono na wabunge karibu wote.
Eneo jingine ambalo limeshambuliwa zaidi ni lile utozaji ushuru wa asilimia 25 kwa magari chakavu, yenye umri wa zaidi ya miaka nane kutoka miaka 10 na zaidi inayotumika hivi sasa.
Waziri Mkuya katika taarifa yake, alisema hatua hiyo ya Serikali, inalenga kudhibiti uingiaji wa magari chakavu, ambayo alidai yamekuwa yakisababisha ajali na kugharimu maisha ya wananchi.
Hata hivyo, wabunge wengi walipinga wakidai kuwa yapo magari hata ya Serikali, yamekuwa yakipata ajali wakati ni mapya, huku wengine wakisema kigezo cha miaka si sahihi kupima uchakavu, bali kigezo sahihi ni kilometa ambazo gari limetembea.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete jana alikutana na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara huyo ambaye ni tajiri mkubwa zaidi barani Afrika, Dangote.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Dangote alimweleza Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kinachojengwa na kampuni yake. 
Dangote alisema kiwanda hicho cha Mtwara kitakuwa kikubwa zaidi kuliko kiwanda chochote cha saruji katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini isipokuwa kinachojengwa Afrika Kusini.
Rais Kikwete amekuwa akiweka msukumo wa kipekee katika ujenzi wa kiwanda hicho kwa nia ya kuongeza uwekezaji nchini na pia kuinua kiwango cha saruji nchini. 
Katika jitihada zake hizo, mwezi uliopita, Rais Kikwete alifanya ziara katika kiwanda kikubwa zaidi kuliko vyote vya saruji katika Afrika kinachomilikiwa na Dangote kilichoko Nigeria.

No comments: