WATU 13,846 WAKAMATWA KWA BIASHARA YA MIHADARATI

Watu 13,846 wamekamatwa kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini katika kipindi cha miaka mitano.
Watu hao wamekamatwa kuanzia Januari mwaka 2009 hadi Mei mwaka  huu. Pia kilo 966.06 za dawa za kulevya aina ya heroini, kilo 363.7 za kokeni , kilo 45,734 za mirungi na tani 212.71 za bangi zilikamatwa katika kipindi hicho.
Vilevile watanzania 178 wanatumikia vifungo mbalimbali nchini china katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka jana huku wengine 113 wamefungwa Brazil hadi Aprili mwaka huu kutokana na kujihusisha na biashara hiyo ya dawa za kulevya na kuhukumiwa nchini humo.
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal aliyasema hayo jana kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani na kubainisha kuwa hali hiyo inaleta taswira mbaya kwa Tanzania kimataifa.
Aidha alisema katika kipindi cha mwaka 2011 hadi Mei mwaka huu kulikuwa na jumla ya watumiaji 1,526 wa dawa za kulevya waliokuwa wanaendelea kupatiwa tiba kwa kutumia dawa aina ya Methadone katika hospitali ya taifa ya Muhimbili,Mwananyama na Temeke.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema vita dhidi ya dawa za kulevya inapaswa kuwa ya watu wote pasipo kubagua umri kwani hivi sasa watu wote wakiwemo watoto wadogo wanatumika katika kusambaza na kusafirisha.
Akitoa ushuhuda wa athari za za matumizi ya dawa za kulevya,bmsanii nguli wa muziki wa kizazi kipya, Rehema Chalamila maarufu kama Ray C mbele ya mamia ya watu waliohudhuria maadhimisho hayo alisema mafanikio makubwa aliyoyapata ikiwemo kujenga nyumba nzuri na ya kisasa akiwa na umri mdogo kutokana na kazi ya muziki yalififia na kubaki historia baada ya kutumbukia katika dimbwi la matumizi ya dawa hizo hatari.

No comments: