WATEJA WA UMEME, MAJI HAWAFAHAMU HAKI ZAOBaraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA CCC) limesema sekta za nishati na maji , zinakabiliwa na changamoto ya watumiaji wa huduma hizo, kutokuwa na uelewa kuhusu haki na wajibu wao, jambo linalotoa mwanya kwa watoa huduma kutowajibika.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA CCC),  Profesa Jamidu Katima, alisema hayo juzi alipotembelea maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, yanayohitimishwa leo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es  Salaam.
Profesa alitaka watoa huduma za nishati na maji, kutumia maadhimisho hayo kuleta chachu ya kuboresha huduma, wanazozitoa ili kuleta maendeleo katika sekta za maji na nishati.
Alisema  kiini cha kero nyingi zinazotolewa na watumiaji wa huduma za maji na nishati, ni kukosekana kwa taarifa na elimu sahihi kutoka kwa watoa  huduma na hivyo kusababisha maswali mengi yasiyokuwa na majibu miongoni mwa watumiaji wa huduma za nishati na maji.
Alitaja baadhi ya kero zinazolalamikiwa na watumia huduma za nishati na maji kuwa ni pamoja na ankara  kubwa za umeme na maji , ambazo haziendani na matumizi halisi ya wateja.
Alisema  mara nyingi malalamiko hutokana na ankara za kukadiria, upatikanaji hafifu wa huduma za maji kwenye maeneo mengi ya miji, kukatizwa kwa huduma bila kutoa taarifa, ucheleweshwaji wa kuunganishwa kwenye huduma husika baada ya kukamilisha malipo stahiki na kauli zisizofaa kutoka kwa baadhi ya watumishi wa taasisi husika.
Aidha, Profesa Katima alieleza kuwa, ingawa mikataba ya huduma kwa wateja ni muhimu kama moja ya eneo linalotathmini misingi ya utawala bora, mikataba hiyo haijawafikia watumiaji wengi wa huduma za maji na nishati. 
Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na EWURA lilianzishwa chini ya Kifungu namba 30 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, Sura ya 414, lengo kuu likiwa ni kutetea na kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za nishati na maji.

No comments: