WANASHERIA 400 KUJIUNGA NA TAASISI YA MAFUNZO


Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) inatarajia kudahili wanafunzi takribani 400 kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, yanayotarajia kuanza Agosti mwaka huu.
Akizungumza juzi Ofisa Mawasiliano wa taasisi hiyo, Scholastica Njozi alisema udahili huo utakuwa ni kundi la 17 la kupata mafunzo kwa vitendo tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo miaka mitano iliyopita.
“ Hadi Juni mwaka huu, tumeshadahili makundi kumi na sita na kupata mafunzo na wengine bado wanaendelea na mafunzo,” alisema.
Taasisi imedahili jumla ya wanafunzi 4,189, wanafunzi 1,107 kati yao bado wanaendelea na mafunzo, wanafunzi 3,082 wamemaliza mafunzo na kufanya mitihai ya Taasisi. Kati ya waliomaliza wanafunzi 1,445 wamefaulu mitihani yote na kupewa tuzo ya stashahada ya uzamili katika utaalamu wa kisheria.
Tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, wahitimu wote wa shahada ya sheria kutoka vyuo vinavyotambuliwa na serikali na vyuo binafsi, wanaotarajia kufanya kazi kama mawakili binafsi nchini au katika utumishi wa umma, hufanya mafunzo ya mwaka mmoja katika taasisi hiyo na kufaulu mitihani.
Njozi alisema lengo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo, ni kuhakikisha haki inamfikia kila Mtanzania na kwa wakati, kwa kuwa mafunzo hayo yanaboresha stadi, ujuzi na viwango vya utendaji kazi wa wanasheria nchini.

No comments: