WAMACHINGA WATAWANYWA KWA MABOMU MWANZA

Polisi  mkoani hapa wamelazimika kutumia mabomu ya machozi  kuwatawanya machinga waliocharuka baada ya kuona vibanda vyao walivyojenga maeneo yasiyoruhusiwa  vikibomolewa.
Machinga zaidi ya 10 wanashikiliwa na Polisi kwa kushiriki katika vurugu  hizo.
Shughuli za kiuchumi na kijamii zilisimama kwa takribani siku nzima huku wananchi waliokuwa wakielekea  mjini wakikumbwa na taharuki.
Mabomu hayo yalianza kurushwa majira ya saa nne asubuhi katika Barabara ya Nyerere na viunga vyake ikiwemo mtaa wa Libert, Msikiti wa Ijumaa, Rwegasore, Makoroboi, Barabara Uhuru, Utemini na Soko la Mirongo ambapo machinga walionekana wakizagaa huku wakati mwingine wakirusha mawe kujibu mashambulizi ya polisi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Chritopher Fuime alisema operesheni ya usafi ilikuwa ikifanyika nyakati za asubuhi katika
eneo la Tempo ambapo baada ya zoezi hilo la kubomoa, baadhi ya Machinga walianza vurugu na kuchoma moto.
“Matangazo ya kuwataka machinga kuondoka kwenye
maeneo yasiyoruhusiwa yametolewa kwa miezi miwili sasa na wapo walioondoka na wengine kukaidi, machinga wanatumia umoja wao vibaya kwani taarifa walikuwa nazo”.
Awali kabla ya jeshi hilo kulazimika kutumia mabomu
ya machozi majira ya saa moja asubuhi  mgambo wa Halmashauri ya Jiji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waliendesha operesheni ya usafi kwa kubomoa vibanda vya wafanyabiashara ndogo maarufu kama machinga.
Zoezi hilo la ubomoaji lililalamikiwa na Machinga hao kuwa limefanyika bila kupewa taarifa hivyo mali zao nyingi kupotea ama kuchukuliwa.
Naye Mlezi wa Shirika la Umoja wa Machinga (SHIUMA), Alfred Wambura alisema ubomoaji unaoendelea ni sehemu ya utaratibu wa Idara ya Mipango Miji ya kuliweka Jiji katika hali ya usafi na halina pingamizi.
Amewataka vijana kutii sheria kwa kufanya biashara katika maeneo yaliyoruhusiwa kwani licha ya zoezi hilo kufanyika machinga hao walipewa nafasi ya kuondoa mali zao.
Hivi karibuni katika Siku ya Mazingira Halmashauri ya Jiji la Mwanza ilipokea tuzo na zawadi mbalimbali kwa kushika nafasi ya kwanza ya usafi kwa majiji kwa mara ya tisa mfululizo.

No comments: