WAHANDISI WAELEZA CHANGAMOTO ZA UADILIFU

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Edwin Ngonyani amesema wahandisi wanakabiliwa na changamoto ya kutakiwa na waajiri wao kufanya kazi kwa matakwa yao na si kufuata taaluma ya kihandisi.
Ngonyani (pichani kushoto) alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano na gazeti hili baada ya kiapo chake kama mhandisi, akiwa mmoja wa wahandisi 250 waliofanya hivyo katika Viwanja vya Karimjee baada ya utaratibu huo kuanzishwa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli mwaka jana.
Alisema wahandisi wengi wanakuwa na nia ya kutekeleza kazi zao kulingana na taaluma zao na kiapo walichokula lakini wanapata shinikizo kutoka kwa waajiri wao jambo linalopekea majengo mengi kujengwa chini ya viwango.
Waziri Magufuli amelazimika kuanzisha kiapo cha utii kwa wahandisi wote nchini kitakachotumika kumfutia leseni ya taaluma Mhandisi mara atakaposhindwa kuwajibika ipasavyo katika kusimamia miradi husika.
Hatua hiyo inatokana na kuwapo na kashfa ya kuanguka kwa baadhi ya maghorofa, ujenzi wa barabara na vivuko usiokidhi kiwango, kwa mujibu wa Magufuli, Serikali haifurahishwi na majengo kuporomoka kwa vile inajenga sifa mbaya kwa wanataaluma hao huku jamii ikikosa imani na taaluma hiyo.

No comments: