WAFANYABIASHARA MCHIKICHINI WAOMBA 'HISANI' YA UBINAADAMU

Wafanyabiashara wa soko la Ilala Mchikichini ambao wanadai kupoteza mitaji yao na kuwaacha na madeni katika taasisi za fedha kutokana na moto ulioteketeza soko hilo wamesikitishwa na kitendo cha serikali kutowajali.
Wafanyabiashara hao wamesema kwamba pamoja na maafa makubwa waliyoyapata hawajaona viongozi wakuu wa serikali wakafika kuwafariji.
Aidha wamesema kwamba wanahitaji muda zaidi wa kulipa madeni yao..
Hata hivyo mfanyabiashara mwingine Lucas Mushi alisema wameweza kuwasiliana na taasisi walizokopa fedha kuwaeleza hali halisi na wameambiwa wasubiri watajibiwa.
Alisema katika mazingira yao magumu wameomba kupewa muda wa nyongeza wa kurejesha mkopo na pia kuangaliwa kama inawezekana waweze kupewa mikopo mingine ili waweze kuinuka tena kibiashara.
Pia  alisema wanashindwa kuelewa ni nini msimamo wa Serikali juu ya soko hilo kwa sababu viongozi wana kauli tofauti juu ya soko hilo.
Aidha alisema hata kama Serikali ilikuwa na mpango wa kuboresha soko hilo basi wangefanya hivyo kabla wafanyabiashara hawajajenga kwa fedha zao au watoe miaka kadhaa ili wafanye biashara kurejesha hali yao ya awali ya biashara ndipo ujenzi mwingine ufanyike.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa soko hilo la Mchikichini, Jumanne Kongogo,  alisema hasara iliyopatikana ndio inasababisha malalamiko yote hayo.

No comments: