Spika wa Bunge la Tanzania, Anne
Makinda ameongoza wananchi wa Mkoa wa Iringa waishio Dar es Salaam kwenye
harambee ya kuchangia Jubilee ya Miaka 25 ya Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa
Jimbo Kuu Iringa.
Katika harambee hiyo iliyofanyika
Dar es Salaam jana, jumla ya Sh milioni 20.2 zilipatikana zikiwa ni ahadi na
fedha taslimu ambazo zitajumuishwa ili kusaidia maendeleo jimboni Iringa.
Akiongoza harambee hiyo, Makinda
alisema ni jambo la furaha kwa watu kuona umuhimu wa kusaidia kazi za maendeleo
ya wananchi na kusema maendeleo ya watu huletwa na watu wenyewe ikiwa
watashirikiana.
Alisema kwa kuona umuhimu wa
harambee hiyo ya Jubilee ya Miaka 25 ya uaskofu wa Ngalalekumtwa ambaye pia
anatimiza miaka 40 ya upadri, yeye na wabunge wa Njombe na Iringa wametoa Sh
milioni 10 kusaidia maendeleo Jimbo la Iringa.
"Mimi na wabunge wenzangu wa
Iringa na Njombe tumeona jambo hili ni jema na kwa umoja wetu tumechangia Sh
milioni 10," alisema Makinda.
Naye Mwakilishi wa Askofu wa Iringa
jijini Dar es Salaam, Padri Luciano Mpoma alisema harambee hiyo itasaidia
kuboresha mahitaji ya maendeleo anayoyafanya Askofu Ngalalekumtwa jimboni
Iringa.
Askofu Ngalalekumtwa, pamoja na kuwa
askofu wa Jimbo la Iringa, pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki
Tanzania. Alipata daraja la upadri mwaka 1973 nchini Italia na mwaka 1988
aliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paul wa pili kuwa Askofu Mwandamizi wa
Jimbo la Sumbawanga.
Hata hivyo, mwaka 1992 alihamishwa
na Baba Mtakatifu, Papa John Paul kuwa askofu wa Iringa nafasi aliyonayo hadi
leo anapotimiza miaka 25 ya uaskofu na 40 ya upadri.
No comments:
Post a Comment