WAASWA KUTOBAGUA WANAOTIBIWA KWA BIMA YA AFYA

Serikali mkoani Kagera imewataka watoa huduma wa idara ya afya kuacha tabia ya kuwabagua wagonjwa wenye kadi za bima ya afya husani wazee pindi wafikapo hospitalini na vituo vya afya kupata huduma.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu Fabian Massawe katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa mkutano wa siku ya wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mjini Bukoba,
Alisema yapo malalamiko ya wagonjwa wanachama wenye kadi za NHIF na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ya kuwa wanabaguliwa wanapokwenda kupata matibabu  kwenye hospitali na vituo vya afya vilivyotengwa kwa ajili ya kutoa huduma hiyo na kuonekana kama wagonjwa wa daraja la mwisho kwa kuwa hawana fedha taslimu.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameliomba Bunge kutunga sheria na pia katika katiba mpya iwemo sheria ya kuwa kila mwanachi ajiunge na NHIF au CHF ili kupata matibabu bora na ya gharama nafuu.
Alisema hiyo itasaidia tabia ya watu kutapatapa wanapougua kiasi cha kugeuka wasumbufu kwa ama ndugu au wenyewe kujikuta wakiuza mali zao kwa bei ya kutupa ili tu wapate fedha za kujiuguzia.

No comments: