VIONGOZI ILALA WACHANGIA DAMU KUOKOA WAGONJWA


Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa na Diwani wa Kata ya Kipawa, Bonnah Kaluwa jana waliwaongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam katika kampeni ya kutoa damu ili kuchangia Benki ya Damu inayokabiliwa na upungufu wa damu.
Tukio hilo kubwa, lilifanyika katika Viwanja vya Sitaki Shari Majumbasita, ambapo viongozi hao walisema wamechukua hatua hiyo kama ishara ya kuonesha kuguswa na vifo, vinavyotokana na ukosefu wa damu vikiwemo vya uzazi.
Akizungumza wakati akitolewa damu, Silaa alisema takwimu zinaonesha kuwa Manispaa ya Ilala, inakusanya asilimia 33 tu ya mahitaji ya damu kila mwaka, kiasi ambacho hakitoshelezi mahitaji ya wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.
“Upungufu huu wa damu unasababisha wakazi wa Manispaa ya Ilala na wakazi wengine wa Jiji la Dar es Salaam kushindwa kupata damu inayotosheleza mahitaji hatua ambayo inasababisha vifo kuongezeka.
“Ni lazima sasa kila kiongozi kwa nafasi yake akawahamasisha wakazi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kutoa damu ili kutunisha benki yetu ya damu iweze kukidhi mahitaji yanayohitajika.
Ni jambo la kupongeza kuona Diwani wa Kipawa (Bonna) ameweza kuandaa hafla kama hii ya leo ambapo idadi kubwa sana ya wakazi wa Dar es Salaam wamefika hapa ili kutoa damu,” alisema Silaa.
Kwa upande wake,  Kaluwa alisema; “ Mimi kama mama, kama kiongozi na kama mzalendo nimeona umuhimu wa kuandaa kampeni hii ili kuwezesha wakazi wa Dar es Salaam kutoka maeneo yote wajitokeze kutoa damu.
“Ni jambo la kutia faraja kuona muitikio umekuwa mkubwa kiasi hiki na ni imani yangu kwamba kiwango cha damu kitakachokusanywa leo kitasaidia sana kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu ambao leo wapo mahospitalini wakiteseka kutokana na kukosa damu,” alisema Diwani huyo.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk Willy Sangu alisema Serikali itaendelea kuwaunga mkono viongozi wanaowahamasisha Watanzania kujitolea damu kwa vile hatua hiyo itasaidia katika kupunguza vifo vya wananchi vinavyotokana na kukosa damu.
Kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam Juni 12, mwaka huu na Diwani huyo na iliweza kudumu kwa muda wa siku 10, kabla ya jana kufikia tamati kwa mafanikio makubwa, kutokana na idadi kubwa ya watu kujitokeza kuchangia damu.

No comments: