UGOMVI WA JAJI WEREMA NA KAFULILA WACHUKUA SURA MPYA

Tafrani iliyojitokeza bungeni juzi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Frederick Werema kumuita Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila(NCCR Mageuzi) tumbili, naye kumjibu kwa kumuita mwizi imeingia katika hatua nyingine ambapo wawili hao wamekataa kusuluhishwa.
Jana asubuhi baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuahirisha shughuli za Bunge, Mwenyekiti wa Bunge, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan 'Zungu', aliwakuta Werema na Kafulila wakiendeleza mzozo nje ya ukumbi wa Bunge.
Kutokana na hali hiyo, Zungu alijitolea kuwapatanisha huku akijaribu kukaa katikati awashikishe mikono ili yaishe, lakini hakufanikiwa.
Wakati Zungu akifanya jitihada hizo, Werema alilalamika. “Mimi nina watoto na wajukuu unanitukana…kwani ninyi hamkusikia akinitukana?” Alihoji huku baadhi ya waandishi wakishuhudia.
Wakati Werema akilalamika kutukanwa huku Zungu akiwa katikati yao, Kafulila naye alilalamika: “Wewe uliniita mimi mnyama (Tumbili) kumbuka vizuri.”
Werema akijibu malalamiko ya Kafulila, alisema yeye hakuwa na nia ya kumtukana bali alikuwa akielezea msemo wa Wanyankole kuwa tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni na kukataa kushikana mkono na Kafulila akisisitiza aombe radhi.
Kutokana na hali hiyo, Kafulila aliondoka kutoka nje ya uzio wa ukumbi wa Bunge bila kuomba radhi huku akimnyooshea kidole Werema, ambaye naye aliingia katika ofisi za Bunge huku akilalamika kutukanwa na Kafulila.
Juzi kabla ya kutoa kauli hiyo, Werema alikuwa akitoa ufafanuzi wa muongozo ulioombwa na Kafulila kuhusu fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT), ambazo zimelipwa kampuni ya PAP, inayomiliki mitambo ya Kampuni ya Independent Power limited(IPTL).
Werema alisema fedha hizo si za Serikali kama inavyodaiwa na Kafulila kwa kuwa fedha za Serikali hazikai katika akaunti hiyo.
Aliendelea kufafanua kuwa taarifa zinazotolewa zinapotosha umma kuwa serikali imetoa fedha kuilipa IPTL, wakati ukweli ni kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo kutokana na misuguano baina ya wanahisa wawili waliokuwa wamiliki wa IPTL. 
Werema alibainisha kuwa mmoja wa wanahisa hao, alikuwa akitaka IPTL ifilisiwe huku mwingine akipinga juu ya jambo hilo mpaka walipouza hisa zao na kumaliza mgogoro huo, ambapo Mahakama iliruhusu mali za kampuni hizo zipewe kwa mwanahisa mpya, PAP.
Werema alisema kuna watu walileta bungeni  vipeperushi wakidai ni ushahidi kuhusu utoaji wa fedha hizo za akaunti ya Escrow na kuhusisha na rushwa.
"Kafulila ni miongoni wanaoeneza taarifa potofu…, kama ni tuhuma au kuna rushwa itakuja kujulikana, tusubiri uchunguzi wa vyombo husika,” alisema.
Wakati akizungumza, Werema alitumia mfano wa kabila la Wanyankole, aliosema kuwa wana usemi unaosema kwamba tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni.
Kabla ya kufafanua maana ya msemo huo, Kafulila bila kuwasha kipaza sauti alikuwa akipiga kelele kumuita Werema kuwa ni mtuhumiwa hivyo atangaze maslahi yake.
“Naomba nisikilize hata kama ni mtuhumiwa nina fursa ya kusikilizwa …nisikilize  wewe tumbili,” alijikuta akisema Werema.
Baada ya kusema hivyo, Kafulila hakukubali na yeye bila kuwasha kipaza sauti alisema: “wewe (Werema) ni mwizi tu.”
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Zungu alimuomba Jaji Werema kukaa chini ili atoe ufafanuzi, huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) na Kafulila wakitaka kuzungumza.
Zungu alisema kwa kuwa Bunge lilishaamua kuwa suala hilo lipelekwe Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ni vyema kama Kafulila ana ushahidi wowote, apeleke huko.
Baada ya kutoa muongozo huo, ambao ulisitisha malumbano, Mwenyekiti Zungu alisitisha shughuli za Bunge mpaka jioni na kuondoka huku akisindikizwa na makatibu wa Bunge na wapambe kama kawaida.
Hatua ya Mwenyekiti wa Bunge kuondoka katika ukumbi baada ya kusitisha shughuli za Bunge, ilimpa fursa Jaji Werema kuweka sawa makabrasha yake na kutoka katika kiti chake, ambapo alionekana kama vile anakwenda kumkabili Kafulila.
Wakati hilo likitokea, Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbai (Chadema), alihama katika kiti chake na kukimbilia alipokuwa amekaa Kafulila.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya mawaziri  walimzunguka Jaji Werema kabla hajamfikia Kafulila na Kasulumbai.
Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro,  Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Abdullah Juma Saadalla na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene.
Nje ya Bunge, Kafulila na Mnyika waliitisha mkutano na waandishi wa habari, ambapo walidai kuwa na ushahidi wa kutuhumu baadhi ya mawaziri kusema uongo bungeni kuhusu fedha hizo za Escrow.

No comments: