Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania
(TMAA) umefanikiwa kudhibiti utoroshaji wa madini yenye thamani takribani Sh
bilioni 15.72 katika viwanja vitatu vya ndege hapa nchini tangu mwezi Julai
2012 hadi Machi 2014 na imeahidi kuongeza kasi ya udhibiti.
Mafanikio hayo ni baada ya Wakala
ulipoanza kukagua wasafiri na mizigo katika viwanja vya ndege katika kipindi
hicho ambapo jumla ya matukio 43 ya utoroshaji wa madini yenye
thamani hiyo yaliripotiwa kwenye viwanja hivyo.
Hayo yalisemwa na Mwezeshaji
wa Wakala, Julius Moshi wakati alipowasilisha mada ya shughuli za
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania kwa washiriki wa semina elekezi kuhusu
ukaguzi na udhibiti wa uzalishaji na mauzo ya madini ya ujenzi na
viwandani yaliyofanyika mjini Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel
Bendera alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina hiyo elekezi ambayo
iliwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wachimbaji, wawakilishi na
wasafirishaji wa madini wanaotumia malori, viongozi wa Serikali ya Mkoa na
wilaya, madiwani, wenyeviti na watendaji wa vijiji vilivyopo kwenye maeneo
yenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Kwa mujibu wa mwezeshaji huyo,
kupitia kaguzi mbalimbali, Serikali imepata mrabaha na takwimu sahihi za madini
yanayozalishwa na migodi mikubwa hapa nchini.
Hata hivyo alisema, Serikali
imeendelea kupata mafanikio mbalimbali ambapo katika kipindi cha kuanzia mwaka
1998 hadi 2013, jumla ya Dola za Marekani milioni 437 zilikusanywa kama
mrabaha kwa kipindi hicho.
Mafanikio mengine yaliyopatikana kwa
kipindi cha Juni 2011 hadi machi 2014, Wakala umewezesha Serikali kukusanya
mrabaha wa jumla ya Sh bilioni 3.6 kutokana na ukaguzi wa madini ya ujenzi na
viwandani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel
Bendera akifungua semina hiyo elekezi alisema, sekta ya madini
kukabiliwa na changamoto nyingi hususani mchango mdogo katika taifa usioendana
na kasi ya ukuaji wake.
Awali, Kaimu Mtendaji Mkuu TMAA,
Mhandisi Dominic Rwekaza alisema Wakala utaendelea kuweka vipaumbele vya
ukaguzi wa shughuli za usimamizi na utunzaji wa mazingira, ukaguzi na uhakiki
wa gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi.
No comments:
Post a Comment