TBL YACHIMBA KISIMA KING'ONG'O

Zaidi ya familia 700 katika mtaa wa Kimara King’ongo Kata ya Saranga,
jijini Dar es Salaam,  zinatarajiwa kunufaika na msaada wa mradi wa kisima
cha maji uliotolewa na Kampuni ya Bia nchini (TBL) .
Akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya  kiasi cha Sh milioni 29 kwa ajili
ya uchimbaji wa kisima hicho juzi, Mwenyekiti wa Mtaa wa King’ong'o
Demetrius Mapesi alisema msaada huo utapunguza uhaba wa maji, unaokabili eneo hilo la Kimara.
Alisema hivi sasa  wakazi wa eneo hilo, wanalazimika kununua maji kwa Sh 500 kwa ndoo moja kutokana na tatizo hilo.
Alisema baada ya kisima hicho, kukamilika watanunua ndoo  moja kwa Sh 100, jambo alilosema ni sawa na faraja  kwao, kutokana na hali ya uchumi ilivyo.
Hata hivyo, aliwaomba wadau wengine kujitokeza kutoa msaada zaidi hususani katika eneo la huduma hiyo ya maji katika mtaa huo, unaokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 116,000.
Alisema pamoja na uwepo wa visima vingine viwili kutoka kwa wafadhili
wengine (Dawasa), bado wananchi wamekuwa wakilazimika kununua maji kutoka kwa wasambazaji binafsi wanaotumia  malori.
Awali, akikabidhi mfano wa hundi hiyo,  Ofisa Uhusiano wa TBL, Doris Malulu
alisema: “Kampuni imeguswa na tatizo linalowakabili wakazi wa eneo hili kwa
muda mrefu na kuamua kuirejeshea jamii sehemu ya kile inachokipata na
kusaidia jamii.
Mhandisi Onesmo Sigalla  kutoka Kampuni ya MO Resources Limited,
alisema  mradi huo unatarajiwa kukamilika katika wiki tatu na aliwataka wananchi kukitunza kisima hicho kitakapokamilika.

No comments: