SUMATRA YATAKA USHIRIKIANO KUDHIBITI KUPAA NAULI ZA DALADALA

Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) kuondoa tatizo la magari ya abiria kupandisha nauli kiholela.
Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray aliliambia gazeti hili jana kuwa baadhi ya magari yanapandisha nauli kiholela nyakati za usiku na kubadilisha ruti kwenda yasikopangiwa jambo linalosababisha wananchi kupata usumbufu wa usafiri wakati huo.
“Kikubwa kinachohitajika ni ushirikiano wa wananchi, wasipoeleza matatizo wanayokutana nayo sisi tutakuwa hatuyafahamu , hivyo watueleze tuchukue hatua,” alisema Mziray.
Alisema kuna baadhi ya magari ambayo tayari wameyakamata kwa ajili ya kupandisha nauli na wamekuwa wakiwatoza faini wale ambao wanakubali makosa na wanaokataa na wakati wametenda tunawapeleka mahakamani.
Alisema wanaokamatwa na kukubali makosa wanatoza faini ya Sh 250,000 ila wanaokamatwa na kukataa hupelekwa mahakamani na hukumu huwa faini ya Sh 500,000 au kifungo cha miezi sita hadi mwaka.

No comments: