Wafugaji wa kuku nchini wataanza kupata neema
ya kupata dawa ya mifugo yao kwa bei rahisi, baada ya Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) kugundua chanjo ya kwanza ya kuku duniani dhidi ya
ugonjwa wa ndui.
Chanjo hiyo ambayo imegunduliwa na mtafiti,
Profesa Philemon Wambura wa SUA, itazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya MCI
Sante Animale ya Morocco katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania. Inatarajiwa
kuanza kusambazwa hivi karibuni ikiuzwa kwa bei rahisi.
Jana SUA ilitiliana saini makubaliano na
kampuni hiyo ya kimaitaifa inayotengeneza dawa na chanjo mbalimbali za mifugo
kutumia matokeo ya utafiti wa chanjo kuku dhidi ya ugonjwa wa ndui.
Makubaliano hayo yalifanyika katika ofisi za makao
makuu ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech); iliyofadhili utafiti
huo ambao umefanywa kwa miaka 10.
Mkurugenzi Mkuu wa Costech Dk Hassan Mshindo
alisema kwa mara ya kwanza kazi za watafiti wa nchini zimeanza kuonekana
kwa kampuni za nje badala ya kukaa kwenye makabati.
Alisema utafiti huo wa Profesa Warioba
utawasaidia wafugaji wa hapa nchini kuweza kuwakinga kuku wao dhidi ya magonjwa
hatarishi ukiwemo ugonjwa wa ndui.
Mwakilishi wa Kampuni ya MCI Dk Baptiste
Dungu, alisema kampuni yake inatengeneza dawa kwa viwango vya kimataifa na
akaeleza kufurahishwa na utafiti wa Profesa Wambura kuwa utakuwa na manufaa
makubwa kwa wakulima wa Afrika na Tanzania.
Kwa upande wake Profesa Wambura, alisema ni
ngumu watafiti wa hapa nchini kupata fedha za kufanyia tafiti kutoka nje ya
nchi hivyo akaeleza kitendo cha Costech kutoa fedha kwa watafiti wa hapa nchini
kutasaidia kazi za watafiti ziweze kuonekana.
No comments:
Post a Comment