SHISHA KILEVI HATARI! HUSABABISHA SARATANI, UGONJWA WA MOYO



Watumiaji wa kilevi cha shisha wako katika hatari kubwa ya kuugua maradhi ikiwemo saratani na kuathirika katika mfumo wa hewa.
Wataalamu wa afya wameonya kwamba ulevi huo ambao kwa sasa umeshika kasi na kuteka watu wengi hasa vijana, una hatari kubwa kuliko uvutaji wa sigara. 
Iinasadikiwa watu wengi, hususani vijana, hivi sasa wameibukia katika uvutaji huo, wakiamini ndiyo mbadala wa  sigara kwa kudhani kuwa haina madhara.
Daktari wa Kitengo cha Matibabu ya  Saratani, Hospitali ya Aga Khan, Dk Amiyn Alidina, alisema hayo  kwenye majadiliano ya ufahamu wa magonjwa ya saratani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Dk Alidina alisema kilevi hicho  hakina tofauti na sigara, ambayo mvutaji wake hawezi kukwepa magonjwa ya saratani, maradhi ya moyo na maradhi ya mfumo wa hewa.
"Shisha haiwezi kuwa mbadala wa sigara kwa kudhani kuwa mtu hawezi kupata saratani na magonjwa mengine, hii ni hatari zaidi," alisema.
Ulevi huo hutengezwa kwa kutumia chombo maalumu chenye bomba la kutolea moshi, ambacho huwekewa tumbaku, maji na moto huku ikiaminika mvuke husaidia kuchuja nguvu ya tumbaku inayoathiri mwili.
Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), mkupuo mmoja wa shisha una kemikali hai  4,800 na kwamba kemikali hizo husababisha saratani ya mapafu, maradhi ya moyo na matatizo katika mfumo wa hewa.
Taarifa hizo za WHO  zinaeleza kwamba,  kiasi cha uvutaji wa shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara kati ya 100 na 200.
Hii ni kutokana na kwamba, mvutaji wa sigara hupata mikupuo kati ya minane na 12 ambayo huingiza lita 0.5 hadi 0.6 za moshi. Lakini kwa upande wa shisha, taarifa hizo za wataalamu zinaonesha anaweza kuvuta mara 200, kiasi ambacho huingiza kati ya lita 0.15 hadi moja ya moshi. 
 Dk Alidina anafafanua kwamba saratani imekuwa tatizo kubwa ambalo kwa kiasi kingine huchangiwa na mtindo wa maisha ambao umefanya watu kushindwa kufahamu utaratibu wa kujikinga. 
Wakati huo huo alisisitiza kwamba iwapo kwenye familia ipo  historia ya  watu wenye saratani, inatakiwa kuwa  waangalifu zaidi. 
Miongoni mwa mambo ambayo jamii na familia kwa ujumla zinasisitizwa kuzingatia, ni ulaji wa matunda  na kuacha matumizi ya pombe na sigara. Mtaalamu huyo pia anahimiza  kufanya mazoezi ili kujiepusha na hatari ya kuugua saratani.
Wakati hapa nchini, hususani  jijini Dar es Salaam, lipo wimbi kubwa la vijana wakiwemo wasichana wanaojihusisha na uvutaji wa kilevi hiki katika baa mbalimbali, vile vile taarifa kutoka maeneo mbalimbali duniani, zinaonesha  kundi hili kutekwa na matumizi ya shisha. 
 “Uvutaji wa shisha unazidi kukua kwa sababu watu wengi hawajui madhara yake kama wanavyofahamu uvutaji wa sigara,” Profesa wa Chuo Kikuu cha London, Robert West, alikaririwa hivi karibuni na gazeti la Daily Mail la Uingereza. 

No comments: