RAIS KIKWTE AAGIZA MSAKO WALIPUAJI BOMU ZANZIBAR



Rais Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki watu wote waliohusika katika ulipuaji bomu lililosababisha kifo na kujeruhi watu saba mjini Unguja, Zanzibar. 
Kikwete ambaye amesema  kitendo hicho ni cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda amani Bara na Visiwani,  amekitaja kuwa ni  cha woga kisicho na ustaarabu,  kisichokubalika katika dunia ya sasa. 
Alisema hayo katika salamu za rambirambi alizotuma jana kwa Rais Ali Mohamed Shein wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 
Bomu hilo lilirushwa katika shughuli ya kidini iliyokuwa ikifanyika katika eneo la Darajani ,  mjini Unguja. Miongoni mwa majeruhi, yumo mhubiri wa amani ajulikanaye kama Sheikh Ahmed Haidari Jabir wa Zanzibar.
“Hicho ni kitendo cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda amani Bara na Visiwani, ni kitendo cha woga na kisicho na ustaarabu na wala hakikubaliki katika dunia ya sasa,” alisema. 
Rais Kikwete aliongeza, “Hiki ni kitendo kilichofanywa na watu waoga, wasio na ustaarabu  wa aina yoyote ile.”
Alikemea wanaofanya vitendo hivyo na akahimiza watu kuwa wastaarabu, wavumilivu na kuheshimu imani na mitazamo ya watu wengine hata kama hawakubaliani nao.
Akiendelea kulaani, alisema amesikitishwa zaidi na watu hao wasio na ustaarabu ambao wamefanya kitendo hicho cha kihalifu kwenye shughuli ya kidini ambapo ndipo mahali panapostahili amani, uvumilivu na unyenyekevu zaidi kwa kuwa ni wakati ambapo binadamu anapofanya mawasiliano na muumba wake.
Alihimiza polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki  wahusika wa tukio hilo. 
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai wa Zanzibar, Yussufu Ilembo, aliyekufa papo hapo ni Muhammad Mkombalaguha (26), mkazi wa Tanga. 
Kutokana na tukio hilo, polisi visiwani humo ilitangaza hali ya hatari watu waliohusika na shambulio hilo. Ilielezwa kwamba uchunguzi umeanzia kwenye mabaki ya vitu vilivyokutwa katika eneo la tukio. 
Miongoni mwa vielelezo vilivyokusanywa ni pamoja na vipande vya mabaki ya gundi ya karatasi na  vitu vingine ambavyo vinasadikiwa vimetumika kutengeneza bomu hilo. 
Mtu aliyekufa pamoja na majeruhi, walikutwa na mkasa huo wakati wakitoka Msikiti wa Darajani baada ya Ibada ya Swala ya Isha inayoswaliwa kuanzia saa 1:45 usiku na kuendelea. 
Baada ya kumalizika ibada hiyo, walitoka msikitini na kufika eneo la Darajani wakisubiri gari na ndipo mlipuko mkubwa uliposikika ambao unasadikiwa kuwa ni bomu.
Katika hatua nyingine, akiwa mkoani Dodoma juzi, Rais Kikwete aliwataka Watanzania kuendelea kulinda na kupigania amani  iliyopo kwa ustawi na usalama wa nchi.
Rais Kikwete alisema hayo juzi  kwenye uzinduzi wa tamasha la uzalendo lililoasisiwa na wasanii wa muziki na filamu nchini ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa video ya wimbo maalumu wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Alisema uzalendo kwa Watanzania ndiyo njia pekee ya kufanya taifa liendelee kutunukiwa hadhi ya kisiwa cha amani duniani.
Katika tamasha hilo lililofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema ili kuwaenzi waasisi wa taifa,  ni lazima  kudumisha misingi ya amani na kujitolea kizalendo kulilinda na kulitetea taifa kama walivyofanya waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Shehe Abeid Amaan Karume.
Pia aliwataka wasanii kutumia vizuri talanta walizojaliwa  kufikisha ujumbe wenye uzalendo  kwa  Tanzania. 

No comments: