PROGRAMU YA MAZINGIRA BORA YA BIASHARA YAKAMILIKA

Programu ya kuwezesha mazingira bora ya biashara (BEST AC) ambayo imedumu kwa muda wa miaka 10 inakamilisha uhai wake kesho.
Programu hiyo ambayo ilikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kufadhiliwa na Serikali za Uholanzi, Denmark, Sweden na Uingereza inabadilishwa na kuwa BEST-Dialogue.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya BEST-AC Michael Laiser kufungwa kwa Programu hiyo kunakaribisha Program nyingine inayowezesha mazungumzo katika Sekta ya Biashara.
BEST AC ilikuwa ni kipengele cha tano cha uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini Tanzania chini ya Ofisi ya Waziri  Mkuu.
Kufungwa kwa kipengele hicho kunafanyika huku kukiwa na mafanikio mengi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004 hasa katika kuonesha changamoto mbalimbali za ufanyaji biashara nchini.
Kwa mujibu wa Laiser, BEST-AC imekuwa ikisaidia taasisi binafsi kuanzisha na kuimarisha ushawishi wa kubadilisha mazingira ya biashara kwa lengo la kuondoa vikwazo na kukuza uchumi.
BEST-AC katika uhai wake imesaidia kuwepo kwa mazungumzo kati ya Sekta Binafsi na Umma, ufanyaji biashara na ubadilishaji wa mfumo na sheria zinazokwaza biashara.
Naye Meneja wa Mradi wa BEST-AC, Hans Determeyer alisema BEST-AC imesaidia taasisi nyingi za watu binafsi kwa kuzipa ruzuku, mafunzo na masuala ya ufundi.
Kwa mujibu wa Hans kwa miaka kumi BEST AC imesaidia kuamsha uelewa, kushawishi kuondolewa kwa kanuni zinazoharibu ufanyaji biashara na kubadili mifumo ya sera na sheria.
Aidha BEST- AC imeshirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na cha Mtakatifu Augustine Mwanza (SAUT) kuboresha utoaji habari za biashara na uchumi na kuanzisha mitandao ya kuwezesha mazungumzo kati ya sekta ya umma na binafsi.

No comments: