Wasomi wengi nchini wameshindwa
kujiajiri kutokana na kutojua kuwa elimu waliyonayo imewafungua akili ili
waweze kufanya mambo yao wakiwa na uelewa mzuri hali inayowafanya kutegemea
vyeti walivyonavyo.
Kauli hiyo ilitolewa hivi
karibuni na Waziri Ofisi ya Rais asiyekuwa na Wizara Maalumu Profesa Mark
Mwandosya alipokuwa kwenye mahafali ya wanafunzi
ambao ni wanachama wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wa vyuo vikuu vilivyopo mkoani Dodoma.
Mwandosya alisema wengi
wamejikuta wamekwama kujiajiri kutokana na kusubiri ajira bila kujua kuwa
elimu waliyopata imelenga kuwasaidia kufanya mambo ya kimaisha kutokana na
uelewa walioupata vyuoni na vinginevyo.
Alisema hivi sasa ushindani
katika soko la ajira ni mkubwa kutokana na wasomi kuwa wengi hivyo ni
afadhali wakaweka malengo ya kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao.
‘’Vijana wangu …
hakikisheni mnajiwekea malengo ya kujiajiri pindi muondokapo vyuoni
maana kukosa malengo kutawafanya kutojituma na kujikuta kila siku mkiuza
vyeti ambavyo kila mtu anavyo badala ya ubora wa elimu mlioupata
vyuoni’’, alisema.
Awali chama cha CCM kilipokea
jumla ya wanachama wapya 230 na kuwakabidhi kadi wanachuo wa Chuo cha Mipango
na Maendeleo Vijijini (IRDP) na wengine sita waliokabidhi kadi wakitokea
Chadema akiwemo kiongozi wao Belina Maingu maarufu kwa jina la Balozi.
Jumla ya wanafunzi 1,500 wa
vyuo 10 vilivyopo mkoani hapa ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi
walikutana kwenye mahafali ya kwanza yaliyowakutanisha kwa pamoja mwaka huu
tofauti na miaka mingine ambayo kila chuo hufanya chenyewe.
No comments:
Post a Comment