NHC YAKABIDHI NYUMBA 40 BENKI KUU

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),  Felix Maagi jana alikabidhi nyumba 40 ambazo zimenunuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) huku akizitaka taasisi nyingine kujitosa kujengewa nyumba na shirika hilo.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa makabidhiano ya nyumba hizo zilizopo eneo la Medeli Manispaa ya Dodoma.
Nyumba hizo zina thamani ya Sh bilioni 4.8 ambapo ni wastani wa Sh milioni 117 kwa kila nyumba.
Alisema taasisi nyingine zinakaribishwa kwa ajili ya kuingia mkataba na NHC ili waweze kujengewa nyumba zenye ubora unaokubalika.
Maagi alisema NHC imejenga nyumba zenye viwango ambavyo BoT walivihitaji na makubaliano ya ujenzi huo yalifanyika mwaka jana na wahandisi wa BoT walipata fursa ya kuangalia wakati ujenzi unaendelea.
Alisema unaponunua nyumba NHC unapata kwa ubora na ukubwa mteja anaouhitaji na kunapunguza gharama kwani unalipa kwa awamu wakati ujenzi unapoendelea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Uendeshaji wa BoT, Leonard Kisarika alisema  walifikia uamuzi wa kujenga nyumba Dodoma kutokana na kuwa na harakati za kufungua ofisi mkoani Dodoma.
“BoT iko kwenye mradi wa kujenga ofisi Dodoma lakini tukapewa changamoto na  bodi kuwa hatuwezi kufungua ofisi bila kuwa na nyumba za kukaa wafanyakazi na katika harakati tukapata mpango wa ujenzi wa nyumba eneo la Medeli tukafuatilia na kuingia nao mkataba,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Usimamizi wa Miradi wa NHC, Haikamen Mlekio alisema mradi mzima una nyumba 150 na Benki Kuu wameweza kununua nyumba 40 ambazo ni za kisasa.
Pia alisema eneo hilo lina huduma mbalimbali ikiwemo maduka na saluni ili kupunguza usumbufu kwa wakazi wa nyumba hizo kwenda umbali mrefu kutafuta huduma hizo.

No comments: