NACTE YAFUNGUA OFISI TANO ZA KANDAWizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi ( NACTE),  imefungua ofisi tano za kanda,  ikiwa ni sehemu ya mkakati wa wizara ya kuwekeza katika eneo la usimamizi wa sekta ya elimu nchini kuongeza ufanisi na kufikia Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Ofizi hizo na makao yake makuu kwenye mabano ni Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Ziwa (Mwanza),   Kanda ya Kusini (Mbeya), Kanda ya Kati (Dodoma) na Zanzibar.
Katika uzinduzi wa kanda hizo, uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,  Profesa Sifuni Mchome  alisema kanda hizo zitaongeza ufanisi na usimamizi wa elimu ya ufundi nchini.
Alisema Wizara itaendelea  kutekeleza mikakati iliyojiwekea  kuhakikisha ubora wa elimu unasimamiwa vema na unalindwa hiyo ikiwa ni pamoja na kukabili watoa huduma kwenye sekta ya elimu wasiokuwa makini.
Alisema utamaduni wa kutegemea ofisi zilizopo makao makuu Dar es Salaam,  unapaswa kurekebishwa  kuwawezesha wananchi kupata huduma katika sekta ya elimu kwa ukaribu zaidi jambo ambalo litawapunguzia pia gharama
Mkurugenzi Mtendaji wa NACTE , Dk Primus Nkwera alisema ofisi hizo za kanda, zitakuwa na majukumu ya kusimamia na kutekeleza mipango na mikakati ya Baraza na Wizara kwa ujumla katika sekta ya elimu ya ufundi nchini ikiwemo udhibiti na usimamizi wa vyuo vya elimu ya ufundi.

No comments: