MUUNGANO WA MAKANISA KUOMBEA KATIBA MPYA

Muungano wa makanisa uitwao Africa Let’s Worship (AFLEWO) umeandaa mkesha wa kusifu, kuabudu na maombi kwa Taifa kwa ajili ya mchakato wa Katiba mpya na Uchaguzi Mkuu mwakani.
Kwa mujibu wa waandaaji wa mkesha huo, utafanyika katika Kanisa la City Christian Center Upanga (CCC), kesho kuanzia saa tatu usiku ukishirikisha waimbaji 50 wa makanisa mbalimbali watakaoimba kwa pamoja jukwaani.
Mchungaji wa Kanisa la International Evangelism Church, Abel Orgenes aliwaambia waandishi wa habari jana jijini hapa kuwa, pamoja na kwamba ni mara ya nne kuandaa mkesha kama huo, lakini huu utakuwa wa tofauti.
Alisema kaulimbiu ya mkesha huo ni “Muacheni Mungu Atawale”. Alisema lengo la mkesha huo ni kuwakumbusha wananchi kuwa Mungu akitawala amani itakuwepo na yote wanayotaka yafanyike nchini, yatafanyika kwa amani.
Naye Mchungaji Safari Paul wa Kanisa la Dar es Salaam Pentecostal Church (DPC) alitoa rai kwa wananchi kuhudhuria kwa wingi kuombea nchi na Afrika kwa ujumla.

No comments: