MMEA UNAODAIWA KUTIBU UKIMWI HATARINI KUTOWEKA



Mmea wa asili unaostawi kwa wingi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, maarufu kwa jina la Chikanda, upo hatarini kutoweka kutokana na kuvunwa kiharamu na watu wanaoamini unasaidia kupunguza makali ya Ukimwi. 
Zao litokanalo na mmea huo linafanana na kiazi mviringo , linadaiwa kuwa na soko kubwa katika nchi za Zambia na Malawi. Tofauti na viazi vya kawaida, katika shina lake Chikanda huzaa kiazi kimoja pekee.
Kaimu Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo iliyopo Matamba wilayani Makete, mkoani Iringa, Pius Mzimbe, alisema uchunguzi waliofanya katika nchi hizo unaonesha viazi hivyo vya Chikanda hutengeneza dawa kwa matumizi ya binadamu na pia kwa ajili ya chakula. 
Akizungumza na wanahabari waliotembelea hifadhi hiyo hivi karibuni, alisema wavunaji haramu huingia kinyemela katika hifadhi hiyo yenye milima mingi na kuvuna mimea hiyo na huuza kwa Sh 80,000 hadi Sh 100,000 kwa debe katika nchi hizo.
Kwa mujibu wa Mzimbe, kiazi cha mmea huo, kipo kwenye kundi la nyara za Serikali na kwamba anayevuna au hata kupanda ndani na nje ya hifadhi akibainika anahesabiwa amefanya kosa la jinai.
 “Yapo madai kwamba watu wanaohitaji aina hiyo ya kiazi kitokanacho na mmea huo wamekuwa wakiwatumia wenyeji wa maeneo haya, kufanya uvunaji huo haramu na hivyo kuathiri uoto wa asili wa hifadhi hii,” alisema.
 Hata hivyo Mzimbe alikanusha kuwepo kwa utafiti wa kisayansi unaothibitisha kwamba mmea huo una uwezo wa kweli wa kuwatibu watu waliopungukiwa na kinga za mwili kutokana na Ukimwi.
 Katika kukabiliana na majangili wanaovuna mmea huo, alisema wanatumia kitengo chao cha ulinzi na intelejensia ambacho kwa kiasi kikubwa kimeanza kufanikiwa kuwadhibiti. 
Mhifadhi wa Utalii katika hifadhi hiyo, Rimus Mkongwe alisema ndani ya hifadhi hiyo kuna aina 40 za mmea huo. Hata hivyo alisema unaotakiwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu ni unatoa majani mawili.
 Alisema taarifa walizonazo kutoka katika nchi  zinazonunua kiazi kitokanacho na mmea huo zinaonesha kwamba kinaliwa zaidi na matajiri wakubwa wa nchi husika. 

No comments: