MKE WA MFALME MSWATI II KUFUNGUA MAONESHO SABASABA

Maonyesho ya 38 ya kimataifa yanayofanyika katika Viwanja vywa Mwalimu Nyerere Kilwa yaliyopo barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yaliyoanza jana yanatarajia kufunguliwa rasmi Jumatano ijayo na Malkia wa Swaziland, Nomsa Matsedula.
Maonesho hayo ambayo kwa mwaka huu yatatembelewa na viongozi mbalimbali wa nje ya nchi,yameanza huku kukiwa na changamoto ya mabanda mengi kutomaliza maandalizi.
Akizungumza na waandishi wa habari,Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara,Uledi Mussa alisema ufunguzi rasmi utafanyika Julai 2, mwaka huu  na kufunguliwa na mmoja wa wake wa Mfalme Mswati II wa nchi hiyo aliyefungua maonesho hayo mwaka jana.
Alisema katika maonesho hayo makampuni 498 kutoka nje ya Tanzania yanashiriki, huku ya ndani yakiwa 1,700, achilia mbali mikoa 10 na mashirika mbalimbali na taasisi 10.
“Maonesho haya ya mwaka huu yanafanyika kwa kuhakikisha kila anayetembelea anapata fursa za kibiashara,mauzo pamoja na kupata mawakala wa biashara nje ya nchi,” alisema
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Jacqueline Maleko alisema katika maonesho ya mwaka huu wameimarisha ulinzi kwa kuweka mashine za CCTV katika maeneo muhimu.
Pia eneo la kuegesha magari limeongezwa,huku kufuatia kugundulika kwa mafuta na gesi nchini makampuni makubw aya nchi wameweka vifaa vyoa ili kuonesha jinsi ya kutumia rasilimali hizo kwa maendeleo ya nchi.
Maleko alisema kuchelewa kwa maandalizi kunatokana na tabia ambayo wamezoea washiriki kwani walitakiwa kuyakamilisha kufikia Juni 25, lakini wengi walikuwa hawajakamilisha malipo hivyo kushindwa kufanya maandalizi hayo.

No comments: