MFANYAKAZI WA TIGO AIBUKA KIDEDEA DUNIANI



Mfanyakazi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo, Obedi Laiser ameibuka kidedea katika shindano la kumtafuta mfanyakazi bora lililoshirikisha wafanyakazi 21 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Marekani ya Kusini.
Amesema ushindi huo kwa hakika si wa kwake au Kampuni ya Tigo pekee bali ni kwa Taifa zima la Tanzania na anajivunia hilo.
Shindano hilo lililofanyika Marekani wiki iliyopita, liliwahusu wafanyakazi kutoka nchi zenye huduma ya mawasiliano chini ya Kampuni ya Mawasiliano na Vyombo vya Habari ya Uswisi ya Millicom. Kampuni hiyo ambayo Tigo ipo chini yake, ndio iliandaa shindano hilo.
Laizer akiwa mmoja kati ya washindani 21 waliochaguliwa kutoka nchi mbalimbali, alisema kuwa ushindi huo si wake tu bali ni wa Taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa ushindi huo unatoa taswira nzuri kuwa Watanzania ni watu wa kuchapa kazi na wanaweza kuwakilisha vema sehemu mbalimbali.
"Haya ni mashindano yaliyoshirikisha wafanyakazi kutoka nchi mbalimbali ambazo zinahuduma za kampuni hiyo ya mawasiliano ya kidigitali ya Millicom sasa kwa hapa Tanzania mimi niliwakilisha nikitokea Tigo na ndio nimeshinda," alisema Laizer.
Laizer aliteuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez kushiriki katika shindano hilo akiwakilisha Tanzania kutokana na ufanyaji wake wa kazi kwa nidhamu.
Gutierrez akizungumzia ushindi huo alisema kuwa hata akiwa katika utendaji wake wa kazi wa kila siku ni mtu mwenye mtazamo chanya katika kila kazi anayoifanya na amestahili tuzo hiyo.
"Ni heshima kwa nchi nzima  kutambuliwa  kama hivi kutoka Millicom, ambaye ni kiongozi wa ulimwengu katika kutoa maisha ya kidigitali na huyu kijana ametoa picha nzuri kwa vijana wengine wa Kitanzania kuwa kumbe wanaweza kufanya kazi zao vema," alisema Gutierrez.

No comments: