MCHIMBAJI MADINI ALAZWA BAADA YA KUJIPIGA RISASI

Mchimbaji madini wa Kampuni ya TanzaniteOne wa Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro katika Mkoa wa Manyara, Mosses Komba (28) anadaiwa kujipiga risasi akiwa ndani ya gari.
Komba ambaye amelazwa kwenye Hospitali ya Arusha Lutherani Medical Center (ALMC), Seliani jijini Arusha kwa ajili ya kupatiwa matibabu, inadaiwa alijipiga kwa bahati mbaya miguu kwa kutumia bastola yake aina ya Brown.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki alisema katika tukio hilo la juzi  saa 3:30 usiku, eneo la  Kazamoyo Kata ya Endiamtu, baada ya kujipiga risasi kwenye paja la kulia, ilitokea  paja la kushoto.
Alisema hawajabaini chanzo halisi cha tukio hilo japo inadaiwa kuwa Komba  alichomoa bastola hiyo baada ya gari lake kugongwa ubavu wa kulia na gari lingine ambalo halikutambulika mara moja.
Alisema Komba alikuwa barabarani eneo la Kazamoyo akiendesha gari aina ya Toyota Celica lenye namba za usajili T 725 CLK, akagongwa na gari lingine ndipo akataka kutoa bastola hiyo ghafla ikafyatuka na kumpiga mguuni.
Kamanda alisema hadi sasa hawajabaini gari lililogongana na  la Komba. Na akasema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo huku wakishikilia silaha hiyo na gari lake pia lipo Polisi kwa ajili ya uchunguzi. 

No comments: