MAWAZIRI WAIPASHA KAMATI YA BAJETI, WASEMA NI KIGEUGEU

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum na Naibu wake, Mwigulu Nchemba, wamehoji utendaji kazi wa Kamati ya Bajeti katika kuzungumzia vyanzo mbadala vya mapato na deni la Taifa sasa.
Wamesema hali hiyo inaonesha jinsi kamati hiyo, ilivyo kigeugeu katika kauli zake.
Akijibu hoja za Kamati hiyo na za baadhi ya wabunge, juzi jioni, Saada aliwataka Wabunge kumunga mkono na pia kuunga mkono Serikali kwa  hatua itakazochukua, baada ya kupokea ushauri wa wabunge kuhusu vyanzo mbadala vya mapato.
Saada alisema anasisitiza hoja hiyo, kwa kuwa mwaka jana, Kamati ya Bajeti ndiyo ilikuwa na hoja ya kutoza kodi katika kadi za simu, lakini wabunge hao hao waliosifu Kamati hiyo, waliigeuka Serikali mpaka kodi hiyo ikaondolewa.
Kwa upande wake, Nchemba alihoji vipi leo Kamati hiyo ya Bajeti inasema deni la taifa ni kubwa, wakati mwaka jana kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri, alipokuwa mjumbe wa Kamati hiyo, walitaka Serikali ikope iwezavyo.
Kwa mujibu wa Nchemba, alipokuwa mjumbe wa kamati hiyo, walipendekeza Serikali ikope hata Sh trilioni 30, ili imalizie miradi ya maendeleo.
Waziri Saada alisema Serikali itaendelea kusisitiza kuwa deni la Taifa ni himilivu na itaendelea kukopa, kwa kuwa haiwezi kutekeleza miradi hiyo kwa mapato ya ndani tu.
Akifafanua kuhusu vyanzo mbadala vya mapato, alisema Serikali haiwezi kuvikubali na kubadilisha bajeti yake, kwa kuwa haijaifanyia utafiti na ni mpaka ikishafanya utafiti, ndio itakubali vyanzo hivyo.
Alitoa mfano wa mapato yanayoelezwa kupotea katika uvuvi wa Bahari Kuu, kwamba Serikali imechukua hoja hiyo.
Lakini, alisisitiza kuwa  itafanya kwanza utafiti hoja hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kabla ya kuichukua na kuitekeleza.
Alimpongeza Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) kwa kusisitiza na kutoa vielelezo vya namna ya kupata mapato katika uvuvi huo. Lakini, alimuomba awe tayari kutoa ushauri wakati wataalamu wa Serikali, watakapomuhitaji.
Katika hatua nyingine, alishangaa kamati hiyo na baadhi ya wabunge, kudai kuwa Bajeti ni ya pombe na soda, wakati vyanzo hivyo vya mapato vinachangia asilimia 0.6 tu ya Bajeti hiyo ya Sh trilioni 19.8
Bajeti ya Serikali ilipita juzi baada ya kuridhiwa na wabunge 234, wakiwemo baadhi ya Kambi ya Upinzani, baada ya kufanyiwa marekebisho kwa kukata fedha kutoka katika matumizi ya kawaida katika maeneo mengi. Walioikataa bajeti hiyo, walikuwa wabunge 66 tu.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Mbunge wa Magu, Dk Festus Limbu (CCM), aliwasilisha taarifa ya mashauriano ya Kamati hiyo na Serikali bungeni, jana, iliyoonesha maeneo yaliyoongezwa fedha.
Dk Limbu alisema katika mashauriano hayo, walikubaliana kukata matumizi ya kawaida na kupata Sh bilioni 165.82, ambazo zilipelekwa katika maeneo yaliyoonekana kuwa na mahitaji zaidi, na kati ya hizo Sh bilioni 34, zilienda katika maendeleo.
Maeneo yaliyonufaika na mabadiliko hayo ni Jeshi la Zimamoto,  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Mengine ni Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Afra na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Uchukuzi, Idara ya Uhamiaji na Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo.
Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi, Waziri Saada, alielezea kuwa kodi ya mishahara itaendelea kupunguzwa katika bajeti ijayo. Katika bajeti ya mwaka 2014/15 kiwango kilichopunguzwa ni kile kile cha asilimia moja, kutoka asimilia 13 mwaka uliopita wa fedha mpaka asilimia 12.
Alisema wakati wafanyakazi wametetewa na wabunge kwa hoja nzito, wasipunguziwe kodi bila kuomba na kushawishi, wafanyabiashara hawataki kulipa kodi, ndio maana alipotangaza vyanzo vya mapato, wote walijazana Dodoma.
Waziri Mkuya alisema ametumiwa ujumbe wa simu, akiambiwa asiende kufuta kodi kwa kuwa ataaibika na kusema, yuko tayari kupigania hatua hiyo ili kodi ilipwe.
Aliwataka wabunge kumuunga mkono wakati wa kufuta misamaha ya kodi na kupambana na matumizi mabaya ya fedha za Serikali yaliyopo mpaka katika halmashauri.
Alitoa mfano wa madeni yaliyowahi kuwasilishwa Hazina ya Sh trilioni 1.5, walipofanya uhakiki wakakuta madai halisi ni Sh bilioni 150.
Pia, alitoa mfano wa mmoja wa watumishi ambaye madai yake yalionesha ni Sh milioni 600, lakini alipoulizwa mwenyewe akashangaa na kutoa risiti, zilizoonesha kuwa anadai Sh 600,000 tu.
Aliwaomba wabunge wamuunge mkono wakati wa kutengeneza sheria ili watumishi wa Serikali wasio waaminifu, wachukuliwe hatua kali za kisheria.

No comments: