KILA KATA TARIME KUPATA GAWIO SHILINGI MILIONI 30

Halmashauri Mama ya Wilaya Tarime yenye Kata 24, imepitisha na kupendekeza mgawo wa sh milioni 30 kwa kila Kata ikiwa ni sehemu ya mgawo wa mrabaha kutoka mgodi wa dhahabu wa North Mara.
Mrabaha huo wa dola 800,000, sawa na sh bilioni 1.2 unatokana na malimbikizo ya deni ambayo mgodi huo ulikuwa nayo kati ya mwaka 2002 na 2005. Aidha, Halmashauri ya Mji wa Tarime iliyogawanywa kutoka Halmashauri Mama ya Tarime, itapata sh milioni 100.
Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi wa Halmashauri Mama ya Tarime, Athuman Akalama katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Halmashauri na kuongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Sylvester Kisyeri.
Akalama alisema: “Tumepata dola laki nane za Kimarekani sawa na shilingi 1,279,200,000, fedha hizo tumezigawa katika makundi 5 yakiwemo ya kumalizia maboma ya majengo ambayo hajayakamilika kama zahanati, madarasa, nyumba za walimu na pia tumezingatia upungufu wa madawati, vitabu vya kufundishia katika shule za msingi na Sekondari. Tutapinguza pia madeni ya wazabuni na watumishi wanaoidai Halmashauri.”
Alisema katika mgawo huo, Kata 24 katika halmashauri hiyo kila moja itapata sh milioni 30.
Baadhi ya Madiwani akiwemo wa Kata ya Pemba, Mgesi Paradiso walitaka madiwani kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuchangia kasi ya maendeleo.

No comments: