MAOFISA ELIMU WAWILI KORTINI KWA KUHUJUMU UCHUMIMaofisa Elimu wawili wa Manispaa ya Tabora na Ofisa Utamaduni, wamefikishwa kujibu mashitaka mawili ya kuhujumu uchumi.
Waliofikishwa mahakamani ni Ofisa Elimu Taaluma,  Rajab Kiteu, Ofisa Elimu Ufundi, Maiko Sawasawa na Ofisa Utamaduni, Madereko Katunzi. 
Walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa  Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Issa Magoli.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Simon Mashingia kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) alidai maofisa hao walitenda makosa hayo Julai mwaka 2011.
Katika shitaka la kwanza, ilidaiwa watuhumiwa wote kwa pamoja wakiwa ni watumishi wa Manispaa ya Tabora, kwa kutumia nyaraka, walimdanganya mwajiri kitendo ambacho ni kosa kinyume na sheria.
Katika shitaka lingine, Mwendesha Mashitaka alidai kila mmoja alimwibia mwajiri Sh 955,000. 
Wote walikana mashitaka hayo na wako nje kwa dhamana hadi Julai 15 mwaka huu kesi itakapotajwa tena. 

No comments: