MAJAMBAZI WAUA POLISI KITUONI NA KUPORA SILAHA


Majambazi wamevamia Kituo cha Polisi Kimanzichana mkoani Pwani, na kuua askari mmoja, D.9887 Koplo Joseph Ngonyani, na kupora silaha tano zenye risasi. 
Silaha hizo ni Shot gun tatu za kiraia na SMG mbili za Jeshi la Polisi.
Tayari Jeshi la Polisi nchini, limelaani na kuanzisha msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wa ujambazi walioua askari huyo kwa kumkata mapanga na kutoweka na silaha zilizokuwa kituoni hapo, katika Wilaya ya Mkuranga. 
Akizungumza jana katika Makao Makuu ya Polisi, jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisema uvamizi huo ulifanyika usiku wa kuamkia jana.
Chagonja alisema watu zaidi ya sita walivamia Kituo Kidogo cha Polisi cha Mkamba na kumshambulia askari huyo pamoja na wengine watatu na kutoweka na silaha hizo.
"Walifika katika kituo hicho na kupora silaha aina ya Shot gun tatu za kirai  na SMG mbili za Jeshi la Polisi zikiwa na magazini zenye risasi 30 kila moja ambazo zilikuwa kwenye ghala la muda kusubiri kupelekwa kwenye kituo kikubwa penye ghala kuu la silaha," alisema. 
 Alisema askari aliyeuawa ni D.9887 Koplo Joseph Ngonyani ambaye alifariki wakati akipata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.
Aidha, alisema watuhumiwa hao pia waliwajeruhi askari mgambo wawili waliokuwa kituoni hapo ambao ni Venance Francis na Mariamu Mkamba ambao wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.
Chagonja alisema jeshi hilo litahakikisha watuhumiwa hao pamoja na silaha hizo zinapatikana haraka kabla hazijasababisha madhara kwa raia wengine. Aidha, aliwataka wananchi kuwa watulivu na kuendelea kushirikiana na polisi wakati upelelezi ukiendelea.
Alitaka wananchi hao kutoa taarifa kupitia namba ya simu ya mkononi ya 0754 785557 au namba za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Ulrich Matei ambayo ni 0715 009953 ili watuhumiwa hao waweze kukamatwa.

No comments: