MADEREVA WATATU WA BODABODA WAFA KWA AJALI



Madereva watatu wa bodaboda wamekufa katika matukio matatu tofauti yaliyohusisha ajali za barabarani.
Katika tukio la kwanza, Ally Omary (29) amekufa papo hapo na abiria wake kupata majeraha baada ya kugongana na gari la kijeshi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 8:30 mchana katika barabara ya New Bagamoyo maeneo ya lango kuu Lugalo Jeshini, Wilaya ya Kinondoni.
Alisema gari la kijeshi aina ya Iveco ambalo halikufahamika namba ya gari hilo na dereva wake, ilitoka upande wa barabara ya Lugalo Jeshini Hospitali na kwenda upande wa pili katika njia isiyoruhusiwa na kugongana na pikipiki yenye namba za usajili T 956 BAH aina ya Skymark.
Alisema dereva huyo wa pikipiki alimpakia abiria aitwaye Ridhiwani Waziri na kwamba pikipiki hiyo ilitokea Mwenge kuelekea njia panda ya Kawe ndipo lori hilo la jeshi lilikatiza mbele yake na kushindwa kuzuia pikipiki hiyo.
Kwa mujibu wa Wambura, dereva wa gari la jeshi alikimbia na gari lake. Majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Lugalo Jeshini na maiti amehifadhiwa hospitalini hapo.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la jeshi kukatiza barabara kwa kutumia njia isiyoruhusiwa.
Wakati huo huo, Abdallah Seif (30) amekufa papo hapo baada ya pikipiki yake kugongwa kwa nyuma na gari lisilofahamika.
Wambura alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 8:03 usiku katika barabara ya Morogoro eneo la mataa Magomeni Wilaya ya Kinondoni.
Alisema gari ambalo halikufahamika lilikuwa likitokea Ubungo kuelekea Kariakoo likiwa na uelekeo sawa na pikipiki yenye namba za usajili T 439 CHU aina ya Fekon iliyokuwa ikiendeshewa na Seif  na kusababisha kifo chake. Maiti amehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika tukio la tatu, dereva wa pikipiki, Ismail Shengwatu (25) mkazi wa Ukonga amekufa baada ya kugongwa na gari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 3:30 usiku  katika barabara ya Mandela maeneo ya Sukita Wilaya ya Ilala.
Alisema gari lenye namba za usajili T 457 AGR aina ya Trailer likiwa na gari lenye namba za usajili T 505 AHD  aina ya Scania likitokea  njia panda ya Tabata  kuelekea Buguruni uelekeo mmoja na pikipiki yenye namba za usajili T 940 CBG aina ya Boxer.
Alisema dereva wa pikipiki hiyo alijaribu kupita lori T 505 AHD na ghafla mbele yake alikutana na gari lililokuwa limeharibika bila ya tahadhari, alijaribu kurudi upande wa kushoto ndipo aligonga Trailer na kufa papo hapo.
Maiti amehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na upelelezi unaendelea.

No comments: