Tanzania ni nchi ya kwanza katika
bara la Afrika kufanya jaribio la chanjo ya ugonjwa wa malaria ambapo watu
watatu waliofanyiwa majaribio ya chanjo hiyo imeonesha mafanikio makubwa.
Chanjo hiyo ijulikanayo kama PfSPZ
Vaccine ilifanyika mwezi uliopita katika Taasisi ya Utafiti wa Afya ya Ifakara
iliyoko Bagamoyo, matokeo ya awali yamethibitisha kwamba chanjo hiyo ni rahisi
na ina uwezo mkubwa wa kuzuia malaria.
Taarifa hiyo ya majaribio ya chanjo
hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Dk Salim
Abdullah pamoja na watafiti wakuu wa malaria Profesa Stephen Hoffman wa Taasisi
ya Sanaria huko Marekani na Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti ya magonjwa ya
kitropiki ya Uswisi, Profesa Marcel Tanner.
"Idadi ya wasomi 73 walikubali
kujitolea katika utafiti huo ambapo mafanikio yake yatasaidia kutokomeza
malaria katika nchi za Afrika, ugonjwa huu unaua zaidi ya watu 600,000 kwa
mwaka kwa Afrika," alisema.
Alisema ilibidi kuchagua wasomi kwa
sababu ni rahisi kwao kuelewa umuhinu wa utafiti huu na kwa kutumia Kituo cha
Utafiti cha Bagamoyo maisha ya watu wakiwemo watoto na watu wazima wataepuka
vifo vinavyosababishwa na malaria.
Dk Abdullah alisema licha ya kwamba
chanjo ya malaria kama hiyo imejaribiwa huko Marekani, utafiti kwa Afrika ni
muhimu kwa jamii katika nchi za joto kwa sababu aina ya malaria huwa ni
tofauti.
Profesa Hoffman alisema vimelea
wanaojulikana kama plasmodium falciparum husababisha malaria kali kwa mgonjwa
na utafiti huu umelenga kueneza chanjo kutokomeza aina hiyo kali ya malaria.
"Tuko katika hatua za awali za
utafiti lakini kutokana na mafanikio hayo mazuri tunaamini chanjo hii itasaidia
kutokoneza malaria kama Polio ilivyotoweshwa duniani," alisema Profesa
Huffman.
Alisema katika kipindi kati ya miaka
mitatu na mitano ijayo, uzalishaji wa chanjo hiyo utakua mkubwa na utasambazwa
katika maeneo mbalimbali duniani ambapo itaokoa watu ambao wangepoteza maisha
kutokana na malaria.
Profesa Tanner alisema pamoja na
chanjo hiyo kusambazwa kwa wananchi bado matumizi ya vyandarua na aina nyingine
ya kujikinga na mbu waambukizao malaria zitaendelea kutumika.
Akitoa shukrani zake kwa watafiti
hao, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Hassan
Mshinda aliwapongeza watafiti hao kwa ushirikiano wao ambao matokeo yake
yatatatua changamoto kubwa ya malaria kwa Tanzania na bara la Afrika.
No comments:
Post a Comment