GAZETI LA MAWIO LATAKIWA KUOMBA RADHI


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya AP Media & Consult Ltd, Peter Keasi ametaka gazeti la Mawio limlipe Sh bilioni mbili kama fidia, kwa kile anachodai kuchapisha habari ambazo zimesababisha kushuka kwa hadhi yake na ya kampuni na hivyo kumwathiri kibiashara.Anatuhumu gazeti hilo, katika toleo la Juni 5 hadi 11 mwaka huu, kuchapisha habari hizo chenye kichwa cha habari  cha ‘CCM kutumia bilioni 3.4 kujitangaza’. 
AP Media & Consult Ltd kupitia Kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza, imetaka gazeti hilo kuomba radhi na wakati huo huo kuchapisha habari kwa usahihi kukanusha upotoshaji na hayo yafanyike ndani ya siku 14 vinginevyo, mhariri wake atafikishwa mahakamani. 
Wakili Kiongozi, Alloyce Komba amemwandikia mhariri wa gazeti hilo la Mawio akisema habari iliyoandikwa, imemdhalilisha na kumkashifu mteja wao. Aidha alisema haikuzingatia maadili ya uandishi wa habari yanayoelezwa na Kanuni za Maadili kwa Wanahabari Tanzania za mwaka 2010 . 
“Mteja wetu ana hadhi kubwa ya kiuongozi, kitaaluma, kibiashara na kitabia pamoja na hadhi ya kampuni yake amesikitishwa sana habari hiyo iliyomshushia hadhi kwa kiasi kikubwa kwani habari hiyo ina taarifa zisizo sahihi, zisizo za kweli na kutoka vyanzo visivyofahamika,” ilisema taarifa hiyo. 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya wakili, pamoja na masuala mengine, habari husika ilisema AP Media ilipewa kazi ya Sh bilioni 3.4 na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukitangaza wakati wa kuelekea sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwake Februari mwakani. Pia ilidai mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo ni mwandishi wa habari wa magazeti ya serikali ya Daily News na HabariLeo. 
“Kampuni haijapewa kazi yoyote kwa zabuni au kuteuliwa peke yake kuitangaza CCM kwa Sh bilioni 3.4…,” ilisema taarifa hiyo iliyokanusha Keasi  kuwa mfanyakazi wa Daily News na HabariLeo kwa kuambatanisha na barua ya kuacha kazi katika Kampuni ya Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) miaka miwili iliyopita. 
Ikinukuu sehemu za habari hiyo, taarifa hiyo ya wakili imesema mteja wao anaonekana ni mhujumu uchumi au ni fisadi kwa wananchi. Ilisisitiza, “mteja wetu hajawahi kuwa mhujumu wa uchumi au kuwa fisadi tangu akiwa mfanyakazi wa shirika la magazeti ya serikali kwa miaka 14 na kupewa hati ya utumishi mzuri .” 
Kuhusu habari ya kusahihisha, gazeti hilo limetakiwa likanushe katika ukurasa wa kwanza wa toleo lijalo kwa kukiri makosa yaliyofanyika kimaadili na kisheria.

No comments: