Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
kwa kushirikiana na nchi wanachama inazifanyia kazi sheria ambazo ni vikwazo
kwa utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja iliyosainiwa mwaka 2010.
Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard
Sezibera alisema mjini Nairobi, Kenya juzi kwamba uhuru wa kufanyakazi,
uhamishaji wa mitaji na bidhaa ndani ya nchi wanachama utawezesha raia ndani ya
kanda kunufaika na itifaki hiyo ipasavyo.
“Sheria zote za kitaifa hazina budi
kuoanishwa ili kuhakikisha kwamba EAC ambayo imebahatika kuwa na rasilimali
nyingi inakuwa mgodi wa kuleta maendeleo,” Sezibera alisema wakati wa mkutano
wa kwanza wa Jukwaa la Biashara la EAC na Ujerumani.
Sekretarieti ya EAC imebainisha
sheria ndogo zaidi ya 6,000 katika nchi wanachama ambazo zinatakiwa kufanyiwa
marekebisho ili kuruhusu utekelezaji wa mtangamano kamili wa EAC.
Vikwazo vya kiuchumi ikiwa ni pamoja
na vizuizi vya barabarani katika njia kuu ya Kaskazini na kati pia limepewa
umuhimu wake.
Katibu Mkuu huyo wa EAC alifafanua
pia kwamba Tanzania imekubali kupunguza idadi ya vizuizi vya barabarani kati ya
Dar es Salaam na Rwanda na Burundi kutoka 15 vya sasa hadi vitatu ifikapo
mwishoni mwa mwaka huu.
Matumizi ya vitendea kazi vya
kielektroniki pia vitapunguza ucheleweshaji wa kupitisha mizigo mpakani,
hususan mizigo inayosafirishwa kwenda nchi zisizo na bahari kama Rwanda
na Burundi.
Rais wa zamani wa Ujerumani, Horst
Koher alisema Ulaya iliwachukua muda wa miaka zaidi ya 40 kulegeza masharti ya
udhibiti wa mipaka.
“Hata hivyo EAC hainabudi kuyakwepa
makosa yaliyofanywa na Umoja wa Ulaya (EU),” alihadharisha wajumbe wa mkutano
huo.
No comments:
Post a Comment